1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine kuanza tena mazungumzo ya amani na Urusi Agosti

Grace Kabogo
18 Juni 2022

Ukraine inapanga kuanza tena mazungumzo ya amani na Urusi mwishoni mwa mwezi Agosti, baada ya kuendesha harakati za kukabiliana na mashambulizi.

https://p.dw.com/p/4CtAt
Türkei Russisch-ukrainische Gespräche in Istanbul
Picha: Sergei Karpukhin/TASS/dpa/picture alliance

Kauli hiyo imetolewa na msuluhishi mkuu wa Ukraine David Arakhamia katika mahojiano yake siku ya Jumamosi na kituo cha Sauti ya Amerika, VOA. Arakhamia amesisitiza kuwa wakati huo, Ukraine itakuwa katika nafasi nzuri kwa mazungumzo.

Wakati vita vikiendelea nchini Ukraine, mazungumzo ya amani yamekwama. Wawakilishi wa Urusi na Ukraine walianza kukutana siku chahce baada ya Urusi kuivamia Ukraine Februari 24. Mwezi uliopita, Urusi iliinyooshea kidole cha lawama Marekani na kusema shinikizo la nchi hiyo limeifanya Ukraine kuvunja mazungumzo hayo.

Hata hivyo, Urusi inadai kuondolewa uwezo wa kijeshi kwa jirani yake huyo na kuachiwa eneo la ardhi mashariki mwa Donetsk na mikoa ya Luhansk.

Ukraine | russisches Kriegsschiff Moskva in Sewastopol
Manowari ya kubebea makombora ya Urusi, Moskva. Picha: Vasily Batanov/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, manowari ya Urusi inayotambuliwa kama Vasily Bech iliyokuwa ikipeleka silaha katika kisiwa kimoja kilichoko katika Bahari Nyeusi, ambacho ni muhimu kimkakati, imezama katika bahari hiyo baada ya kushambuliwa na makombora ya Ukraine.

Taarifa hiyo ambayo haikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru, imetolewa jana jioni na Gavana wa kijeshi wa Odessa, Maxym Marchenko. Hata hivyo Urusi haikuzungumzia tukio hilo. Vasily Bech sio meli ya kwanza ya Urusi kuharibiwa katika vita hivi.

Urusi ilithibitisha kuipoteza meli ya Saratov na manowari yake kuu ya kubebea makombora ya Moskva. Mamlaka ya ulinzi wa mipakani ya Umoja wa Ulaya, Frontex imesema jana Ijumaa kuwa, tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, zaidi ya watu milioni 5.7 wa Ukraine wamekimbilia katika nchi za Umoja wa Ulaya huku wengine milioni 2.8 wakirejea nchini mwao.

(DPA, AFP, Reuters)