1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Waliokufa katika jiji la Kremenchuk waongezeka

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
28 Juni 2022

Idadi ya vifo kutokana na shambulio la Urusi katika eneo la maduka kwenye jiji la Kremenchuk nchini Ukraine imeongezeka na kufikia watu 20.

https://p.dw.com/p/4DNS4
BG Angriff auf Einkaufszentrum in Krementschuk
Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Gavana wa mkoa wa Poltava, Dmytro Lunin,  amesema zaidi ya asilimia 60 ya kifusi kwenye eneo hilo la maduka kimeondolewa ikiwa ni siku moja baada ya eneo hilo kupigwa kombora na kusababisha uharibifu mkubwa ambao umelazimu zoezi la  uokoaji kufanyika. Kulingana na mamlaka ya jiji hilo, watu 59 wamejeruhiwa na wengine kadhaa bado hawajulikani waliko. Meya wa jiji hilo la Kremenchuk Vitaly Maletsky ametangaza kipindi cha maombolezo cha siku tatu.

Raia wakishuhudia eneo la maduka likiteketea kwa moto baada ya kushambuliwa
Raia wakishuhudia eneo la maduka likiteketea kwa moto baada ya kushambuliwaPicha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Wasimamizi wa eneo hilo la maduka wanachunguzwa kwa madai ya kushindwa kuchukua hatua za haraka baada ya kupokea tahadhari kutoka kwenye mfumo wa kutoa taarifa za dharura juu ya uvamizi wa anga, hali iliyosababisha kutochukuliwa hatua za haraka za kuwahamisha watu kutoka kwenye jengo hilo lililoshambuliwa. Wakati huo huo waendesha mashtaka wa nchini Ukraine wamesema uchunguzi wa uhalifu wa kivita umeanzishwa.

Urusi imedai kwamba lengo halisi la shambulio hilo lilikuwa ghala la kuhifadhia silaha kutoka nchi za Magharibi lililopo mbali kidogo upande wa kaskazini mwa maduka yaliyoharibiwa, lakini mlipuko kwenye ghala hilo ndio ulizusha moto kwenye maduka hayo.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema leo kwamba Urusi lazima iwekwe kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi baada ya shambulio la kombora kwenye eneo la maduka lililojaa watu katika jiji la Kremenchuk. Amesema Urusi inaishambulia nchi yake kwa mujibu wa mikakati iliyopanga kuilenga miundombinu ya raia. Rais wa Ukraine amesisitiza kwamba ulimwengu unaweza na kwa hivyo ni lazima uchukue hatua za komesha ugaidi wa Urusi.

Msemaji wa ikulu ya Urusi Dmitri Peskov
Msemaji wa ikulu ya Urusi Dmitri PeskovPicha: Shamil Zhumatov/AFP/Getty Images

Msemaji wa ikulu ya Urusi Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa Habari kwamba Urusi itasitisha mashambulizi yake mara tu Ukraine itakapojisalimisha, na kuitaka serikali ya Ukraine iwaamuru wanajeshi wake kuweka chini silaha zao.

Hapo jana Jumatatu, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema wakati bado haujafika kwa nchi yake kufanya mazungumzo na Urusi na msemaji wa ikulu ya Urusi alipoulizwa kutoa maoni yake kuhusu kauli ya Zelensky, Peskov alisema na hapa namnukuu: "Tunaongozwa na kauli za rais wetu, operesheni maalum ya kijeshi inakwenda kulingana na mipango ya Urusi na tunaendelea kuyafikia malengo yetu." Mwisho wa kumnukuu.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alipozungumza na viongozi viongozi wa G7 kwa njia ya video.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alipozungumza na viongozi viongozi wa G7 kwa njia ya video.Picha: Tobias Schwarz/AFP

Kwa ombi la Ukraine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha mkutano wa dharura mjini New York leo hii kujadili shambulio hilo la Urusi ambalo lilitokea wakati viongozi wa nchi za Magharibi wakiahidi kuendelea kuiunga mkono Ukraine na mataifa hayo makubwa kiuchumi duniani yametayarisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi, ikiwa ni pamoja na kuweka udhibiti wa kiuchumi na kikomo kwa bei ya juu ya mafuta na ushuru wa juu unaotozwa bidhaa mbalimbali.

Vyanzo: DPA/AFP