Ukosefu wa maadili katika kampuni za kutengeneza simu | Masuala ya Jamii | DW | 25.02.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Ukosefu wa maadili katika kampuni za kutengeneza simu

Mwaka 2012 kampuni ya Apple ilikiri kuwa baadhi ya washirika wake wa biashara wananyanyasa wafanyakazi. Hii ni baada ya kashfa ya maelfu ya wafanyakazi kujiua kuikumba kampuni ya Foxconn nchini Taiwan.

Huku makampuni makuu ya kuunda simu za mkononi duniani yakiandaa tamasha mjini Barcelona kuonyesha simu bora zaidi maarufu kama Crème de la Crème, wanaharakati wa haki za kibinadamu wanailaumu sekta hiyo kwa kupuuzia ukiukaji wa haki za kibinadamu unaofanywa katika makampuni ya simu nchini Uchina na kwenye machimbo ya madini nchini Congo.

Yanayoendelea nyuma ya sekta hiyo ya kisasa na inayokua ni unyanyasaji wa wafanyakazi, au madini yaliyojaa matone ya damu kutoka maeneo yenye machafuko. Hayo ni kwa mujibu wa afisa wa shirika la SETEM linalojumuisha mashirika 10 yasiyo ya kiserikali yanayoendesha kampeni ya maonyesho mbadala yenye taswira ya kukuza maadili.

Foxconn Angestellte Fabrik Apple IPhone China

Wafanyakazi ndani ya kiwanda cha Foxconn

Ni makampuni machache tu miongoni mwa washiriki katika kongamano hilo la simu ulimwenguni yaani Mobile World Congress (MWC) ambayo yameonyesha simu zao za kisasa “The Fairphone 2” ambayo kampuni ya Uholanzi inajaribu kuitengeneza kwa kuzingatia maadili.

Kulingana na meneja wa utangamano na umma, Daria Koreniushkina, kufuata mikondo ambayo madini ya kuunda simu hufuata si rahisi. Mkondo huo hujumuisha zaidi ya wahusika mia moja duniani, na kwa kila madini yanayotumika hupitia hatua zisizopungua tano. Hivyo ni changamoto kubwa kuhakikisha kila hatua ni salama.

Njia mbadala ya kutengeneza simu kwa kutii maadili

Katika simu yake ya kwanza, kampuni hiyo lilitumia madini aina ya tin na tantalum kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, madini yaliyohusishwa na mapigano nchini humo. Katika simu yao ya pili iliyozinduliwa mwaka 2015, kampuni ya Fairphone ilitumia madini ya dhahabu kutoka Peru.

Katika viwanda vyake vilivyopo Uchina, kampuni hiyo inaendesha miradi ya usalama wa uundaji simu kwa wafanyakazi wake, kando na kuchapisha majarida kuhusu maslahi ya wafanyakazi. Koreniushkina asema hawawezi kupata kampuni salama katika bara la Asia kimiujiza, lakini uwazi na kuwa tayari kukumbatia njia salama ni mwanzo mzuri kwa kampuni kujiboresha.

Kulingana na shirika la Electronics Watch ambalo linaendesha kampeni ya kuboresha masilahi ya wafanyakazi katika viwanda vya kutengeneza vifaa vya elektroniki ulimwenguni, wafanyakazi wengi katika viwanda vya simu nchini Uchina wanafanya kazi kwa zaidi ya masaa 80 kwa wiki, na wanalipwa mishahara ya chini huku wakiwa katika hatarini kupata madhara ya saratani.

Mwaka 2012 kampuni ya Apple ilikiri kuwa baadhi ya washirika wake wa biashara wananyanyasa wafanyakazi. Hii ni baada ya kashfa ya maelfu ya wafanyakazi kujiua kuikumba kampuni ya Foxconn nchini Taiwan, kampuni inayoitengenezea kampuni nyengine kubwa ya Marekani vifaa vya simu.

Sekta ya kutengeneza simu ina faida kubwa sana. Mwaka jana sekta hiyo ilipata dola trilioni 3 nukta moja. Hiyo ni kwa mujibu wa waandalizi wa maonyesho ya simu mjini Barcelona. Joseph Maria Royo ambaye ni mtafiti katika Chuo Kikuu cha Barcelona anakadiriwa kuwa sekta hiyo itachukua nambari ya nne ulimwenguni katika ukubwa wa kukuza uchumi. Hivyo anahimiza wazingatie maadili ya utu. Royo ambaye ni msomi wa vita vya kujihami, pia ni mdau katika shirika moja dogo lisilo la serikali linaloshutumu jinsi sekta ya kutengeneza simu inavyochangia mapigano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, taifa linaloongoza katika kuchimba madini ya Cobalt na Coltan. Madini hayo ni ya muhimu sana katika kutengeneza simu za kisasa maarufu kama "smartphones"

Unyanyasaji wa watoto kuchimba madini kutengeneza simu

Cobaltmine Demokratische Republik Kongo SPERRFRIST

Watoto wanaochimba madini Jamhuri ya Kijemokrasia ya Congo

Kulingana na shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo huzalisha zaidi ya nusu ya madini ya cobalt ulimwenguni kote. Asilimia 20 ya madini hayo huchimbwa katika machimbo ya muda mfupi na wengi wa wafanyakazi ni watoto wakati mwingine wakinyanyaswa.

Shirka la Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, linakadiria kuwa takriban watoto 40,000 hufanya kazi katika machimbo hayo. Wengine waliohojiwa wana umri wa miaka saba na wanasema hawajawahi kuliona jua kwa siku nyingi kwani wanashinda na kukesha migodini. Wanakosoa makampuni ya simu kufahamu unyanyasaji huo lakini yakajitia hamnazo.

Kwa mantiki hiyo, kampuni ya Fairphone inataka kuwa kileleni kuongoza mchakato wa kukuza maadili katika sekta ya utengenezaji simu. Watu 60,000 katika mataifa ya Ulaya walinunua simu zake za kwanza, huku simu zake 30,000 za toleo la pili tayari zikiwa zimeshanunuliwa. Koreniushkina anasema kwa kuonyesha kuwa watu wengi zaidi wanataka simu salama na zinazozingatia maadili kwenye utengenezwaji wake, wanaweza kuhimiza sekta nzima ulimwenguni kote kuzingatia maadili katika bidhaa zao.

Mwandishi: John Juma/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com