1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa Umoja wa Ulaya mashariki ya kati kuhusu mashambulizi Gaza

Jane Nyingi5 Januari 2009

Licha ya shinikizo kutoka jamii ya kimataifa kuitaka Israel kusitisha mashambulizi katika ukanda wa gaza bado imeyaendeleza.

https://p.dw.com/p/GSR9
Familia ya kipalestina ikitoroka mashambulizi gazaPicha: AP

Idadi ya wapalestina waliofariki kufuatia mashambulizi hayo yaliyowalenga wapiganaji wa kundi la hamas imefikia 523.Tayari viongozi kadhaa wa umoja wa ulaya wamewasili katika eneo la mashariki ya kati kuanza juhudi za kuyasitisha mashambulizi hayo.


Viongozi hao miongoni mwao waziri wa mashauri ya kigeni wa ufaransa Bernard Kouchner,kamishna wa umoja wa ulaya Benita Ferrero walder na Javier Solana wanatarajiwa kuzuru Jerusaleum,Ramallah na Amman kwa mashauri ya kujaribu kusitisha mashambulizi katika ukanda wa gaza.


Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo wa umoja wa ulaya bw.Ferrero waldner kwa mara nyingine amesema mataifa wanachama wa umoja huo wanataka kupatikana kwa suluhu la haraka kuhusu gaza,kwani wanaoendelea kuumia ni karibia wenyeji millioni 1.5 wa eneo hilo.


Wapalestina wanaoishi katika ukanda wa gaza kwa sasa hawana maji, umeme, chakula kimepungua na hata huduma za matibabu zimekuwa matatizo kwani hospitali nyingi hazina dawa na zinatumia genereta.


Solana amesema umoja wa ulaya uko tayari kuchukua nafasi yake kama msimamzi wa eneo la mpakani kati ya Misri na Ukanda wa gaza. Baada ya mashauri na rais wa Misri Honsy Mubarak, huko Sharm el Sheikh, ujumbe huo wa umoja wa ulaya umeelekea Israel.

Katika mahojiano na waandishi wa habari waziri wa maswala kigeni wa Israel Zipi Livni ameleza msimamo wao kuwa hawako tayari kusitisha mapigano na lengo lao ni kuwaangamiza kabisa wapiganaji wa kundi la Hamas.

“Ningependa kusema naelewa kiwango cha uwiano kinachohitajika. Naamanisha kuwa hamas ,wiki iliyopita walilenga shule, wanawalenga raia. Sisi hatutafanya hivyo.Kwa hivyo hatua tunazochukua ni kuwafanya waelewe kuwa mashambulizi hayo dhidi ya raia wa israel yanapaswa kusitishwa. Sisi tunajaribu kuwalinda raia wetu.Kwa hivyo swala la uwiano nadhani linatumika vibaya dhidi ya Israel.'

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy pia anatarajiwa kuwasili katika eneo la mashariki ya kati.Sarkozy kwanza atakutana na rais wa Misri Hosni Mubarak.

Hata hivyo hakuza kueleza bayana iwapo juhudi zake za kujaribu kuishawishi Israel kukomesha mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa kundi la hamas katika ukanda wa gaza zitafua dafu.

Nao viongozi ulimwenguni wamendelea kueleza wasiwasi wao kuhusu mzozo wa kiutu Gaza.rais wa China Hu jinato katika mazumguzo kwa njia ya simu na rais George Bush wa marekani amesema mzozo huo kati ya palestina na Israel huenda ukaathiri eneo zima la mashariki ya kati.

Israel imekanusha kuwa kuna mzozo wowote wa kiutu katika eneo la gaza kufuatia mashambulizi ambayo yamesesababisha vifo vya zaidi ya wapalestina 523 wakiwemo watoto 87.Zaidi ya watu 2500 pia wamejeruhiwa tangu kuanzishwa kwa opresheni hiyo na Israel siku kumi zilizopita.


Wanajeshi wa Israel wanaendesha mapambano ya ardhini, angani na eneo la baharini huko Gaza. Nao wapiganaji wa kundi la hamas yamefanya mashambulizi ya karibu roketi 500 na kurusha makombora tangu kuanzishwa kwa mashambulizi na Israel tarehe 27 mwezi uliopita.