1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wasitisha kuondoka Kongo

10 Julai 2024

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo utasitisha kwa muda mchakato wake wa kuondoka nchini humo.

https://p.dw.com/p/4i6YC
DR Kongo | MONUSCO | Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa KongoPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo hakuna tarehe kamili iliyowekwa ya kuanza kwa awamu ijayo baada ya ile ya kwanza kukamilika mwezi Juni. Hayo ni kwa mujibu wa serikali na ujumbe huo. 

Mnamo Septemba mwaka jana, Rais Felix Tshisekedi aliuomba ujumbe wa MONUSCO kuharakisha utaratibu wa kuwaondoa walinda amani waliopelekwa katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati kutuliza machafuko yanayosababishwa na makundi yenye silaha yanayopigania udhibiti wa maeneo na raslimali.

Balozi wa Kongo katika Umoja wa Mataifa Zenon Mukongo Ngay amesema kuwa awamu ya kwanza ya kuondoka, katika mkoa wa Kivu Kusini, ilikamilika Juni 25. Awali ilitarajiwa kukamilika mwezi Aprili. 

Soma pia:Kongo yaandaa mkutano wa kilele wa kuiboresha misitu barani Afrika

Akizungumza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ngay alidokeza kuwa masharti bado hayajatimizwa kwa ajili ya awamu ijayo, hata hivyo, huku akiilaumu nchi jirani Rwanda kwa kuongezeka kwa machafuko katika eneo la mashariki ya Kongo.

"Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itatetea uhuru wa mipaka yake, mamlaka yake, na usalama wa wakazi wake kwa gharama yoyote ile huku ikiwa wazi kwa utatuzi wa kisiasa wa mzozo na Rwanda kupitia njia za kidiplomasia. Hata hivyo, njia hii itaaminika iwapo tu wanajeshi wa Rwanda watajiondoa kwa ufanisi katika eneo la Kongo ili kuruhusu mazungumzo ya kweli na yenye kujenga.”

"Kwa kuzingatia kuendelea kwa uchokozi wa Rwanda huko Kivu Kaskazini, awamu inayofuata ya kujiondoa, awamu ya pili, itafanywa wakati hali itakaporuhusu, kufuatia tathmini zinazoendelea za pamoja," alisema Ngay.

UN na Kongo waituhumu Rwanda

Kongo na Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu zimekuwa zikiituhumu Rwanda kwa kuliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo Kigali inayakanusha. 

Wanajeshi wa MONUSCO wajiandaa kuondoka DRC

Bintou Keita, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa, anasema hakuna ratiba kamili ya askari wa MONUSCO kuondoka katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri.

"Mambo hayako hasa tunapotaka sote yawe, kuendana na mpango wa kujiondoa; Kwa hivyo, tutachukua muda kutathmini kile ambacho kimefanywa huko Kivu Kusini, kwa kuelewa kwamba serikali itaendelea kuongeza uwezo wake, hasa kupeleka vikosi vya usalama. Alisema Bintou

Naye Waziri wa Mambo ya kigeni wa Kongo Therese Wamba Wagner amesema serikali inataka kuepuka kuweka ombwe la usalama.