1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa matumaini katika ulimwengu unaotisha

17 Mei 2010

Mkutano uliowaleta pamoja waumini wa madhehebu mbali mbali mjini Munich na uchaguzi wa viongozi wapya wa chama cha "Die Linke" ni baadhi ya mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu.

https://p.dw.com/p/NPvL

Basi tutaanza na gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN linalosema:

"Mkutano huo mjini Munich, kusini mwa Ujerumani, umeonyesha jinsi binadamu wengi walivyokuwa na hamu kubwa ya kusikia ujumbe utakaowapa matumaini katika ulimwengu unaotisha. Kwani uporaji wa maliasili na mazingira unahatarisha maisha yao; mifumo ya masoko inawanufaisha wachache wakati wanaoathirika ni wengi mno. Katika dunia ya hivi sasa, ni nadra kutimiza malengo ya waumini wanaotaka kuona amani,haki na upendo."

Gazeti la BADISCHE NEUESTE NACHRICHTEN likiendelea na mada hiyo hiyo limeandika:

"Huo haukuwa mkutano wa kuutaka umma wa Kikristo kutubu. Mivutano mbali mbali, hasa kuhusu mapadri wa Kikatoliki, ni miongoni mwa mada zilizojadiliwa, lakini haikugubika vikao vya mkutano huo. Hiyo huenda ikawa ni thibitisho la mwanya unaozidi kupanuka kati ya waumini na viongozi wa makanisa au pia yaweza kuwa ishara ya imani ya Wakristo katika ulimwengu wa mabadiliko na hofu."

Tukiendelea na uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani, sasa tunatupia jicho mkutano mkuu wa chama cha "Die Linke" uliofanywa mwishoni mwa juma lililopita katika mji wa Rostock, mashariki ya Ujerumani. Mkutano huo,ulichagua viongozi watakaowarithi kigogo Oskar Lafontaine na mwenzake Lothar Bisky ambao ni waasisi wa "Die Linke" chama kinachofuata sera kali za mrengo wa kushoto. Gazeti la SAARBRÜCKER ZEITUNG limeandika:

"Huo ni urithi wa chama kilichogawika: wamashariki walio na mawazo yakinifu na wamagharibi wenye misimamo mikali. Suala linaloulizwa ni iwapo, chama cha "Die Linke" kitaweza kudumu kwa kuendelea kuwa na misimamo miwili mbali mbali. Upande mmoja unaamini kuwa ubepari unaweza kurekebishwa. Upande mwingine unaamini kuwa ubepari kwanza lazima utoweke kabla ya wafanyakazi na wakulima kuweza kupata haki zao."

Na kwa kumalizia, gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE linasema:

"Kwa sasa,hakuna anaeweza kusema iwapo Gesine Lötzsch na Klaus Ernst waliochaguliwa kukiongoza kwa pamoja "Die Linke" wataendeleza au watatokomeza mafanikio ya chama hicho. Viongozi hao wapya hawana vipaji wala fasaha ya Oscar Lafontaine."

Mwandishi:P.Martin/DPA

Mhariri:Othman,Miraji