#UjerumaniYaamua: Barabarani kuelekea uchaguzi | Uchaguzi wa Ujerumani 2017 | DW | 16.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

UJERUMANI YAAMUA

#UjerumaniYaamua: Barabarani kuelekea uchaguzi

Miji sita, waandishi wawili, suali moja kubwa: Kipi kinachowahangaisha sana Wajerumani kuelekea uchaguzi mkuu wa shirikisho wa mwaka 2017? Sumi Somaskanda na Nina Hase wanaandama njia kusaka majibu.

Ripoti za DW kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao wa Ujerumani zimepewa jina la "#UjerumaniYaamua". Je, Wajerumani wataamua muelekeo upi wanaotaka nchi yao iufuate?

Hicho ndicho ambacho waandishi wetu wawili, Sumi Somaskanda na Nina Hause, wanataka kukijuwa kwenye safari yao ya wiki sita ya kuripoti kote nchini Ujerumani iliyoanza katikati ya Juni, ambapo kila wiki wanajikita kwenye kuchunguza mada moja mahsusi kwa eneo moja mahsusi.

Safari yao ilianza tarehe 12 Juni mjini Berlin kuelekea mji wa Dresden wakiwa kwenye basi la Volkswagen likiwa na maandishi yanayosomeka "Ujerumani yaenda wapi?" ubavuni. 

Lengo ni kuanzisha mdahalo na watumiaji wa mitandao ya DW juu ya masuala ambayo yataamua uchaguzi wa Septemba 24, na kutoa majibu kwa maswali ambayo dunia inataka kujuwa kutoka Ujerumani.

Miji sita, maswali sita

Maswali ambayo Sumi na Nina wanayauliza na kuyajadili na watu wanaokutana nao yako namna hii:

"Kundi la siasa kali za mrengo wa kulia lina nguvu gani?" linaulizwa mjini Dresden na viunga vyake.

"Je, bado wakimbizi wanakaribishwa?" ni swali linalochunguzwa mjini Wegscheid na maeneo mengine ya Bavaria.

"Je, uchumi wa Ujerumani uko tayari kwa siku zijazo?" linaulizwa mjini Stuttgart na viunga vyake.

"Je, Uislam unaibadilisha Ujerumani?" uchunguzi wake unafanyika mjini Cologne na viunga vyake.

"Kwa namna gani Ujerumani ina usawa na uadilifu?" linaulizwa mjini Bremen.

Na suala la mwisho kabisa litaulizwa na kuchunguzwa kwenye mji mkuu, Berlin, ambalo litaamuliwa na yale yanayojitokeza sasa safarini kwa lengo la kuuchochea mjadala wa kijamii ambao utakuwa bado unaendelea.

Kwenye kiini cha yote ni umma

Jambo la muhimu la kuzingatia hapa ni kwamba shabaha kuu ya ripoti hizi za televisheni na mtandaoni itakuwa ni watu wa Ujerumani na kile wanachokiona cha maana zaidi kwao katika maisha yao ya kila siku. Mahojiano na wanasiasa na wataalamu yataweka uzito zaidi kwenye ripoti hizo.

Waandishi wetu wanatazamia kuitumia vyema fursa hii ya kuripoti kutoka kwenye maeneo ambayo hayapewi uzito sana nchini Ujerumani kwenye uchaguzi mkuu.

Matukio ya hivi karibuni kwenye siasa za kimataifa, hasa uchaguzi wa Marekani na kura ya maoni ya Brexit nchini Uingereza, yameonesha namna ilivyo muhimu kwa vyombo vya habari kuyaripoti maoni na hisia za watu nje ya miji mikubwa.

Watu wanaweza kuwafuata waandishi wetu kila siku kwa lugha zote mbili, Kiingereza na Kijerumani, wakitumia majukwaa ya mitandao ya kijamii ya Twitter, Facebook Live na Instagram. Matokeo ya uchunguzi wao yatapatikana pia kwenye DW-TV.

Waandishi wenyewe

Sumi Somaskanda amekuwa na Idhaa ya Kiingereza ya DW tangu mwaka 2001 na ana miaka kadhaa ya uzoefu akiwa mwandishi wa televisheni na wa mtandaoni. 

Alizaliwa Rochester, New York, akasomea Chicago na kufanya kazi San Fransisco, kabla ya kuja Ujerumani kwa ufadhili wa masomo wa Bosch akiwa mwandishi wa habari na kusalia kwenye mji mkuu, Berlin, kwa miaka tisa sasa.

"Ikiwa na zaidi ya wakaazi milioni 80, Ujerumani kamwe haishindwi kunishangaza kwa mchanganyiko wake wa kupendeza kabia - sio tu wa kijiongrafia, bali pia wa kijamii, kitamaduni, na hata lahaja."

Alipoulizwa kwa nini safari hii ni muhimu, Somaskanda alielezea dalili za mgawanyiko miongoni mwa wapigakura wa Ujerumani. "Kimsingi, ukiangalia utafiti wa maoni, Wajerumani wanaonekana wanazidi kugawika kuelekea uchaguzi wa mwaka huu - ila nataka kuona ikiwa hivyo ndivyo hasa ilivyo na kwa nini. Nataka kujuwa nini hasa kitawasukuma wapigakura kwenye vituo hapo Septemba, au kuwazuia wasipigekura kabisa."

Tangu mwaka 2005, Nina Hase amekuwa akifanya kazi kama mwandishi, mhariri wa mtangazaji wa Idhaa za Kijerumani na Kiingereza za DW. Alizaliwa kwenye jimbo la North Rhine-Westphalia, baina ya miji ya Ruhr na Münster. 

Kwake, suali halisi kabisa ni namna mfumo wa kisiasa wa nchi yake ulivyotulia. "Kila mahala, ramani ya kisiasa inabadilika, miungano mikongwe inahojiwa - angalia suala la Brexit na uchaguzi wa Marekani - na wanasiasa chaguzi wakitumia kampeni za kupingana na mifumo iliyopo. Kwa upande mwengine, vyama vya kikale vya Ujerumani ni sehemu ya maadili ya jamii ya Kimagharibi."

Kinyang'anyiro cha aina yake

Angela Merkel amekuwa akipewa lakabu ya "kiongozi wa dunia huru" na vyombo vya habari vya kigeni. Mshindani wake mkuu, Martin Schulz, ni mtetezi mkuu wa Umoja wa Ulaya kwenye siasa za Ujerumani. 

"Lakini pia unakiona chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD, kikishinda viti kutoka jimbo moja hadi jengine. Hivi hali ya kutoridhika imefika umbali gani nchini Ujerumani? Una nafasi nzuri ya kujibu swali hili kama unazungumza na watu," anasema Hase.

Mwandishi: Martin Muno/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman


 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com