Ujerumani yatumia diplomasia kushinda vita Afghanistan | Habari za Ulimwengu | DW | 17.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Ujerumani yatumia diplomasia kushinda vita Afghanistan

Wanajeshi wa Kijerumani walioko kwenye jimbo hatari la Kundus wanajaribu kutafuta masikizano na wenyeji wa Ki-afghani, kama njia ya kupambana na uasi wa kundi la Taliban.

Jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan

Jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan

Katika kituo cha kijeshi cha mjini Kundus zaidi ya wanajeshi 100 wa Kijerumani wanafanya kazi pamoja na wanajeshi wa Kimarekani na polisi wa Kiafghani. Lakini kazi kwenye kituo hiki si kumsubiri tu adui wa kundi la Taliban kupambana naye.

Panapokuwa hapana mapambano ya moja kwa moja na adui, basi wanajeshi wana kazi nyengine ya kufanya, nayo ni kutafuta njia za kumshinda adui wao bila kupigana naye. Mkuu wa kikosi cha mafunzo cha Ujerumani, Matthias L. anasema kwamba tangu zamani wamekuwa na uhakika na wanalolifanya.

"Panapokuwa hapana jambo la kufanya, kikosi changu huwa kwenye hatari zaidi kuliko pale tunapokuwa na la kufanya. Hapa tunaposema hapana la kufanywa, haimaanishi kuwa hakuna linalotokea." Anasema Matthias.

Walinda amani wa Ujerumani katika jimbo la Kundus, Afghanistan

Walinda amani wa Ujerumani katika jimbo la Kundus, Afghanistan

Na ndio maana hubidi kufanya kazi ya kulitafuta hilo linalotokea. Na njia mojawapo ya kulipata ni wanajeshi hao wa Kijerumani kutembeatembea mitaani katika wilaya mbaya, kiusalama, kama hii ya Char Darah, bila ya kujua jaala gani inayowangojea, kama ni ucheshi wa wanavijiji au bunduki za Taliban. Lengo ni kujikusanyia taarifa na ikibidi kuzungumza na wapiganaji wa Taliban na viongozi wao. Lakini huko si kujitakia mauti ya makusudi?

Matthias anasema kwamba sio kuwa wanapendelea kujiingiza kwenye hatari, lakini mafanikio ya jeshi la Ujerumani tangu lilipoojingiza Afghanistan mwaka 2002 yametokana kwa njia hii.

Jina la operesheni hii ni Halmasag kwa Kipashtun, ambayo ina maana ya "Umweso." Kwa kushirikiana na wanajeshi wa Kimarekani, Kibelgiji na Kiafghani, wanajeshi wa Kijerumani wameweza kuvikomboa vijiji vingi kutoka mikono ya Taliban kwenye wilaya hii ya Char Dahar.

Kila usiku, utasikia mngurumo wa helikopta zikiruka kwenye anga la Kundus na zinazojiendesha wenyewe zikielekea kwenye vijiji vya jimbo hili, jambo ambalo limeongeza hali ya usalama.

Akizungumzia kuboreka kwa hali ya usalama kwenye eneo lake, mkuu wa polisi wa jimbo hili, Abdul Rahman Sayeed Khili, anasema kwamba kuna sababu tatu, ikiwemo kwanza operesheni iliyopangwa kimahesabu, ambayo kila siku inasonga mbele.

"Pili ni mazungumzo na wapiganaji na makamanda wao ambao huwa tunawavuta upande wetu. Na tatu ni baridi."

Ni kweli kwamba, kwa kawaida katika majira kama haya ya baridi, wapiganaji huwa wako mafichoni, lakini ni kweli pia kusema kwamba Operesheni Umweso, ambayo inawatoa wanajeshi kwenda mitaani kuwashinda maadui kwa kutumia diplomasia na sio silaha, imefanya kazi kubwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Kai Künster

Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

 • Tarehe 17.11.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QBRd
 • Tarehe 17.11.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QBRd
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com