Ujerumani yatoka sare na Cameroon | Michezo | DW | 03.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Ujerumani yatoka sare na Cameroon

Ujerumani ilitoka goli moja nyuma na kulazimisha sare ya magoli mawili kwa mawili na Cameroon, katika mechi ya kirafiki kabla ya Kombe la Dunia na kuonyesha kuwa bado ipo kazi ya kufanywa

Wajerumani ambao watajipima nguvu na Armenia Juni 6 katika mechi yao ya mwisho ya kirafiki mjini Mainz kabla ya kuelekea Brazil, walionekana kwa kiasi Fulani kuwa wadhaifu wakati wakilenga kumaliza kiu ya miaka 18 ya kunyakuwa taji la dunia, huku wakiwakosa wachezaji kadhaa akiwemo nahodha Philipp Lahmna mlinda lango nambari moja Manuel Neuer.

Kocha wa Ujerumani Joachim Löw, ambaye anakitaja kikosi chake cha mwisho cha wachezaji 23 watakaoiwakilisha nchi alisema mchuano dhidi ya Cameroon ulionyesha kazi ambayo bado wanastahili kufanya.

Alisema walikosa ukakamavu na kuonyesha uchovu mwingi lakini hilo ni jambo la kawaida baada ya kuwa katika kambi ya mazoezi kwa siku kumi.

Kocha wa Cameroon Mjerumani Volker Finke aliridhika na matokeo na mchezo wa vijana wake wa Indomitable Lions, akisema wachezaji wanane au tisa kati ya kikosi kilichocheza mechi dhidi ya Ujerumani, wataanza mechi yao dhidi ya Mexico.

Magoli yote manne yalifungwa katika kipindi cha pili wakati Samuel Eto'o alipowaweka kifua mbele The Indomitable Lions. Thomas Müller alisawazisha dakika chache baadaye kabla ya Andre Schürrler kuwapa uongozi Ujerumani. Lakini Eric-Maxim Choupo-Moting alifunga ili kuwaepushia Cameroon kichapo cha pili mfululizo baada ya kushindwa na Paraguay magoli mawili kwa moja Alhamis iliyopita. Ujerumani imepangwa katika kundi G pamoja na Marekani, Ghana na Urengo.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri: Josephat Charo