1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatinga nusu fainali Kombe la Mabara

28 Juni 2017

Ujerumani wamefuzu katika nusu fainali ya kombe la Mabara baada ya kuebuka na ushindi wa 3-1 walipocheza na Cameroon Jumapili huko Urusi. Sasa watakutana na Mexico mjini Sochi.

https://p.dw.com/p/2fW6S
Russland FIFA Confederations Cup - Deutschland vs. Kamerun
Picha: Reuters/G. Dukor

Mfumo wa kumsaidia muamuzi wa mechi kutoa maamuzi yake kupitia video, ulimulikwa kwa mara nyengine baada ya muamuzi kuchanganyikiwa na kumpa mchezaji kadi nyekundu kimakosa.

Muamuzi kutoka Colombia Wilmar Roldan alimshauri muamuzi msaidizi mda mchache baada ya dakika sitini za mechi, kufuatia Ernest Mabouka wa Cameroon kumchezea vibaya Emre Can wa Ujerumani na baada ya tukio hilo, Sebastian Siani ndiye akaishia kupewa kadi baada ya muamuzi kukosea. Wachezaji wa hao the Indomitable Lions walimshinikiza Roldan kuangalia upya tukio hilo na ndipo alipotambua kwamba amefanya makosa na akaifuta hiyo kadi nyekundu aliyompa Siani na akampa Mabouka.

Russland FIFA Confederations Cup - Deutschland vs. Kamerun
Vincent Aboubacar alifunga bao la Cameroon Picha: Reuters/G. Dukor

Kocha wa Cameroon Hugo Broos anasema hafahamu lililotokea na hakuwa katika nafasi ya kujibu lolote kuhusiana na tukio hilo baada ya mechi. "Nafikiri kila mmoja amechanganyikiwa, pia mimi. Sikujua kilichotokea. Kwanza niliona kadi nyekundu, kisha nikaona ya njano. Kisha muamuzi akaja kwa msaidizi wake nje ya uwanja, kisha akarudi uwanjani na kumuonesha mchezaji mwengine kadi nyekundu. Kwa hiyo usiniulize hasa kilichotokea, kwangu mimi ni jambo ambalo sikulielewa na hata sijalielewa hadi sasa. Lakini nadhani hili ni suala la muamuzi mwenyewe."

Cameroon kusalia wachezaji kumi bila shaka ni jambo lililowagharimu mechi kwani Ujerumani waliebuka an ushindi baada ya Kereem Demirbay kuwaweka kifua mbele kisha mshambuliaji wa klabu ya SC Freiburg Timo Werner akaongeza mabao mawili na kuyafanya mabao kuwa matatu huku The Indomitable Lions wakipata bao la kufutia jasho kupitia kwa Vincent Aboubakar.

Russland FIFA Confederations Cup 2017 Chile - Australien
Chile watapambana na Ureno katika nusu fainaliPicha: Reuters/J. Sibley

Kocha Joachim Löw alisherehekea ushindi wake wa 100 na timu ya Ujerumani katika mechi 150 alizozisimamia. "Wachezaji walikuwa na motisha kila mara na baada ya miaka sasa, wachezaji wamekuwa sana kimchezo. Naeza kusema, ukiangalia miaka kumi au kumi na moja iliyopita, na ukilinganisha hali tuliyo nayo na tuliyokuwa nayo wakati huo, lazima nisema kwamba nafurahishwa na mechi hizi 100 nilizoshinda, lakini lazima niwashukuru wale walioambatana nami katika safari hii na hasa nawashukuru sana wachezaji wangu."

Katika mechi nyengine iliyochezwa jana Chile walipewa kitisho na Australia ingawa walifanikiwa kutoka sare ya bao moja na hao the Kangaroos. James Troisi aliwafungua Australia bao katika dakika ya 42 kisha mabingwa wa Copa America Chile wakasawazishiwa na Martin Rodriguez.

Sasa kinyang'anyiro hicho cha Mashirikisho kimeingia hatua ya nusu fainali ambapo Jumatano Ureno wakiongozwa na Cristiano Ronaldo watakuwa wanapambana na Chile kisha Alhamis, Ujerumani wateremke dimbani kupambana na Mexico. Kwa uchambuzi zaidi wa kombe hili la mashirikisho na hatua lililofikia

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFPE
Mhariri: Josephat Charo