Ujerumani yateleza dhidi ya Ufaransa | Michezo | DW | 14.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Ujerumani yateleza dhidi ya Ufaransa

Ujerumani imekubali kipigo cha mabo 2-0 dhidi ya Ufaransa na Uingereza nayo ikagaragazwa na Uhispania kwa mabao 2-0 katika michuano ya kirafiki jana Ijumaa (13.11.2015).

Fußball Länderspiel Frankreich - Deutschland

Wachezaji wa Ufaransa wakishangiria bao

Mabingwa hao wa kombe la dunia Ujerumani waliteleza kwa kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wa fainali za mwakani za kombe la mataifa ya Ulaya Ufaransa katika mchezo ambao uligubikwa na shambulio la risasi mjini Paris pamoja na miripuko karibu na uwanja wa Stade de France, wakati Uhispania nayo ikainyoa Uingereza kwa mabao 2-0 katika usiku wa michuano hiyo ya kirafiki.

Terror in Paris

Mchezo kati ya Ufaransa na Ujerumani ukiendelea wakati taarifa za shambulio zikitokeza

Ubelgiji ikishika nafasi ya kwanza katika orodha ya FIFA ya timu bora kwa sasa iliishinda Italia kwa mabao 3-1, wakati Uholanzi iliyoshindwa kufuzu kucheza fainali za mwakani za kombe la mataifa ya ulaya , iliibwaga Wales iliyofanikiwa kukata tikiti ya fainali hizo kwa mabao 3-2.

Na michezo mingine kwingineko , Poland iliishinda Iceland kwa mabao 4-2, Slovakia ikashinda mpambano wake dhidi ya Uswisi kwa mabao 3-2, Jamhuri ya Cheki ikawa mshindi dhidi ya Serbia kwa mabao 4-1, Ireland ya kaskazini ikaitungua Latvia kwa bao 1-0, Uturuki ikaishinda Qatar kwa mabao 2-1 na Luxemburg ikaishinda Ugiriki kwa bao 1-0.

Frankreich Paris Schießerei Explosion

Shambulio la risasi; wahudumu wakitoa huduma ya kwanza kwa wahanga wa shambulio mjini Paris

Kipigo baada ya michezo 16

Uingereza ilijikuta ikipokea kipigo chake cha kwanza katika michezo 16 kwa mabao 2-0 dhidi ya wabingwa watetezi wa kombe la mataifa ya Ulaya Uhispania mjini Alicante.

"Tulicheza dhidi ya timu nzuri sana. Ilikuwa hali tuliyoitarajia," kocha wa Uingereza Roy Hodgson amesema.

Mchezaji wa kati wa Uhispania Cesc Fabregas amesema : " tulistahili, tumecheza kandanda safi. Tulishambulia kila wakati."

Fußball Länderspiel Frankreich - Deutschland

Mlinzi wa Ujerumani Mats Hummels na Paul Pogba wakiwania mpira

Wahanga wa Heysel wakumbukwa

Mjini Brussels , mchezo wa kirafiki kati ya Ubelgiji na Italia ulisimamishwa katika dakika ya 39 na kukaa kimya kwa muda wa dakika moja kuwakumbuzka wahanga 39 raia wa Italia waliofariki katika ajali iliyotokea katika uwanja wa Heysel miaka 30 iliyopita.

Fußball Länderspiel Frankreich - Deutschland

Mchezo wa kirafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani katika uwanja wa Stade de France

Shambulio baya mjini Paris liligubika mchezo muhimu wa kirafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani uliohudhuriwa na rais Francois Hollande wa Ufaransa na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, ambapo baadaye rais wa Ufaransa alitangaza amri ya hali ya hatari na kusema anafunga mipaka ya nchi hiyo.

Miripuko ilisikika ndani ya uwanja wa stade de France katika kitongoji cha St Denis, kaskazini ya Paris, ambako fainali ya kombe la mataifa ya Ulaya mwakani itafanyika. Mabao ya Ufaransa yalitiwa kimiani na Oliver Giroud na Andre-Pierre Gignac.

Mwandishi: Sekione Kitojo

Mhariri:Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com