Ujerumani yatamba katika dimba la ligi ya mataifa ya Ulaya | Michezo | DW | 15.11.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Ujerumani yatamba katika dimba la ligi ya mataifa ya Ulaya

Timu ya taifa ya Ujerumani imepata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ukraine katika pambano la mechi za ligi ya mataifa ya Ulaya Nations League.

Mabao ya Ujerumani yalipachikwa wavuni na Leroy Sane na Timo Werner aliyefunga mabao mawili.

Kulikuwa na mashaka iwapo mechi hiyo ingechezwa baada ya wachezaji wanne wa Ukraine kukutikana na virusi vya Corona baada ya kufanyiwa vipimo mnamo siku ya Ijumaa.

Wachezaji hao ni Andrii Yarmolenko, Serhii Sydorchuk, Viktor Kovalenko na Viktor Tsyhankov.

Kocha wa Ujerumani Joachim Low aliweka kikosi imara katika pambano hilo wakiwemo wachezaji kadhaa wa Bayern Munich kama vile Leon Goretzka, Leroy Sane, Niklas Sule, Serge Gnabry na mlinda lango mzoefu Manuel Neuer. Pia alimjumuisha beki wa PSV Eindhoven Philipp Max, aliyeichezea Ujerumani mechi ya kwanza katika ushindi wa 1-0 dhidi Jamhuri ya Czech mnamo siku ya Jumatano.

Kwengineko timu ya taifa ya Uhispania ilitoka sare ya 1-1 na Switzerland katika mechi nyengine ya kundi hilo.

Kufuatia matokeo hayo, Ujerumani inaongoza kundi hilo ikiwa na alama 9 ikifuatiwa na Uhispania yenye alama 8, Ukraine ni ya tatu ikiwa na alama 6 nayo Switzerland iko mkiani mwa kundi hilo ikiwa na alama 3.

Ujerumani itakutana na Uhispania siku ya Jumanne mjini Seville, Uhispania huku hatma ya atakayeliongoza kundi hilo ikijulikana baada ya mechi hiyo.