Ujerumani yapata kiti kwa miaka miwili Baraza la Usalama | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.10.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yapata kiti kwa miaka miwili Baraza la Usalama

Ujerumani imepata kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka miwili.

German Foreign Minister Guido Westerwelle attends the vote for non-permanent members for a two-year term on the security council at United Nations headquarters in New York USA, 12 October 2010. Germany, Portugal and Canada are competing for the remaning two seats on the United Nations security council. EPA/PETER FOLEY

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle kwenye kikao cha kuwachagua wanachama wa muda wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Uamuzi huo ulipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika duru ya kwanza ya uchaguzi hiyo jana. Kwa hivyo,miaka miwili ijayo, Ujerumani itakuwa ikihudumia baraza hilo lenye ushawishi mkubwa katika Umoja wa Mataifa. Ujerumani haitoweza kuleta mageuzi makubwa hivyo katika Baraza la usalama, kwani mfumo wa baraza hilo hautoi nafasi ya kufanya hivyo. Mataifa matano makuu yenye kura ya turufu yaani Marekani,Urusi,China, Ufaransa na Uingereza ndio yalio na usemi wa mwisho. Hata hivyo,waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ana sababu ya kufurahi kupata kiti hicho kwa miaka miwili.

Safari ya mwisho, Ujerumani ilipohudumia baraza hilo kama mwanachama wa muda, Marekani ilitaka vita vya Iraq vihalalishwe kimataifa. Lakini jitahada hizo hazikufanikiwa kwa sababu ya upinzani wa Ujerumani iliyokuwa na mashaka yake kuhusu uhalali wa vita hivyo. Wanachama wa muda wana umuhimu, kwani maazimio yanaweza kupitishwa tu ukipatikana uwingi wa kura tisa katika baraza hilo lenye wanachama 15. Mbali na hilo, Ujerumani pia ina ushawishi katika Baraza la Usalama kwani taifa hilo kubwa tayari lina miundo mbinu inayohitajiwa kwa jukumu lake jipya. Ukihesabiwa ule wakati ambapo DDR ilikuwemo katika baraza hilo la usalama, basi mwakani itakuwa mara ya sita kwa Ujerumani kuwa na kiti katika baraza hilo.

Kama mwanachama katika Baraza la Usalama Ujerumani ina nafasi nzuri ya kuongoza, hasa katika suala linalohusika na mabadiliko ya tabia nchi. Hiyo ni mada iliyo muhimu sana kwa nchi za visiwa - na kampeni ya Ujerumani ilihusika na suala hilo. Kwani katika barua iliyopelekwa Umoja wa Mataifa, nchi za visiwa zinataka hatua zichukuliwe kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Panapkuwepo vitisho vya mafuriko na ukame, na binadamu wanapolazimika kuhama makwao, basi mabadiliko ya tabia nchi ni suala linalohusika na usalama wa kitaifa.

Ujerumani katika mwaka 2012 itakuwa pia na fursa ya kuzipa msukumo mada zingine zilizo karibu sana na waziri wa nje Westerwelle: kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia ulimwenguni na kumaliza mizozo katika Mashariki ya Kati. Makubaliano ya kutokuwepo silaha za nyuklia katika eneo la Mashariki ya Kati yanatazamiwa kupatikana kwenye mkutano utakaofanywa wakati huo. Lakini hiyo ni mada tete, kwani ulimwengu mzima unaamini kuwa Israel inadhibiti silaha za nyuklia ingawa nchi hiyo haikukiri hivyo. Vile vile, Israel ni miongoni mwa mataifa matatu ambayo hayakutia saini mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyuklia. Na katika mzozo wa silaha za nyuklia na Iran, Ujerumani tayari inajadiliana na mataifa matano yenye kura ya turufu, bila ya mafanikio. Hata hivyo miaka miwili ijayo,Ujerumani itaweza kupiga kura yake yenyewe katika maazimio yote.

Mwandishi:Bergmann,Christina/ZPR

Mpitiaji: M.Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com