1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yapanua operesheni dhidi ya maharamia

Admin.WagnerD11 Mei 2012

Bunge la Ujerumani limepitisha uamuzi wa kupanua operesheni yake ya kupambana na maharamia katika pwani ya Somalia. Sasa wanajeshi wanaweza kuwashambulia maharamia hao katika nchi kavu na si wakiwa majini tu.

https://p.dw.com/p/14ti8
EU-Mission Atalanta
EU-Mission AtalantaPicha: picture-alliance/dpa

Operesheni ya wanajeshi wa nchi za Umoja wa Ulaya wanaoilinda pwani ya Somalia inafahamika kwa jina la Atalanta. Jana wabunge wa vyama tawala vya Ujerumani, yaani chama cha Christian Democratic Union, CDU, na chama cha waliberali, FDP, walipiga kura ya kukubali kuongezwa kwa operesheni ya Atalanta. Hata hivyo vyama vya upinzani vilipiga kura ya kupinga uamuzi huo. Uamuzi uliopitishwa jana unawapa wanajeshi wa Ujerumani haki ya kuwashambulia maharamia hata katika nchi kavu. Hata hivyo, wanajeshi hao wanaruhusiwa kuingia kiasi cha kilometa mbili tu kutoka ufukweni na kushambulia ghala za maharamia kwa kutumia helikopta au ndege za kijeshi.

Bunge la Ujerumani limepitisha pia uamuzi wa kuongeza muda wa operesheni ya kupambana na maharamia inayoongozwa na Umoja wa Ulaya. Hadi kufikia mwezi Mei mwaka 2013, wanajeshi wapatao 1,400 watakuwa wakipiga doria katika meli za kijeshi na kukamata meli zilizotekwa na maharamia wa Kisomali au meli za maharamia wenyewe. Kwa njia hiyo, Umoja wa Ulaya unataka kuhakikisha kwamba shehena za chakula cha msaada kunachopelekwa katika nchi za pembe ya Afrika kinawafikia walengwa. Mbali na hayo, Umoja huo unataka kurejesha hali ya usalama kwenye njia ya usafiri katika Bahari ya Hindi.

Bunge la Ujerumani, Bundestag
Bunge la Ujerumani, BundestagPicha: dapd

Westerwelle atetea uamuzinwa serikali

Akiyatetea maamuzi ya serikali yake ya kupanua operesheni ya Atalanta, waziri mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, aliwaambia wapinzani bungeni: "Operesheni hii inahusika na kutafuta njia salama za kusafirisha chakula. Ni muhimu kuendeleza operesheni hii," alisema waziri huyo. "Ninasikitika kuona kwamba ninyi mmekataa kuendelea kupigana na maharamia kwa sababu za kisiasa. Ninatumaini kuwa hii si ishara ya kwamba wapinzani wanafuata njia nyingine katika siasa za nje. Ninatumaini kwamba mtatambua ukweli wa mambo."

Waziri wa mabo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido WesterwellePicha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo, Westerwelle alisisitiza kuwa wanajeshi wa nchi yake hawatakanyaga nchi kavu ya Somalia. Maharamia walioko katika nchi kavu watashambuliwa kutoka angani. Kiongozi wa chama cha walinda mazingira, Die Grünen, katika bunge, Bw. Jürgen Trittin, ameeleza kwamba suala la kuishambulia nchi kutoka angani ni la hatari sana, na ndiyo maana chama chake hakikuunga mkono uamuzi uliopitishwa jana.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/afp

Mhariri: Othman Miraji