1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaondoa wanajeshi Inchirlik

Lilian Mtono
7 Juni 2017

Serikali kuu ya Ujerumani ya Kansela Angela Merkel imedhinisha kuhamishwa kwa wanajeshi wake waliopo katika kambi ya jeshi la anga ya Incirlik iliyopo Kusini-Mashariki mwa Uturuki na kuhamishiwa Jordan

https://p.dw.com/p/2eGxr
Türkei Incirlik
Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Hatua hiyo inafuatia kuzorota kwa mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizo. Kansela Angela Merkel alisema uamuzi huo utaziwezesha Ujerumani na Uturuki kuweka kando mojawapo na mizozo inayosababisha mfarakano kati ya washirika hao wawili wa Jumuiya ya kujihami ya NATO.  

Wanajeshi wa Ujerumani wapo katika kambi ya Incirlik, iliyopo karibu na mpaka wa Syria, kama sehemu ya mkakati wa kukabiliana na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, lakini Uturuki iliweka zuio kwa wabunge wa Ujerumani kuitembelea kambi hiyo. 

Ziara za wabunge huchukuliwa kwa umuhimu kwa kuwa upelekwaji wa wanajeshi wa Ujerumani huhitaji idhini ya bunge kabla ya kufanyika maamuzi. 

Vikosi hivyo vinataraji kuanza kuhama kutoka Incirlik kuelekea Jordan baadae mwezi huu. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen amepatiwa mamlaka ya kuratibu zoezi hilo kwa kushirikiana na washirika kutoka Jumuiya ya kujihami ya NATO kuhusiana na namna zoezi hilo la kuhamisha wanajeshi litakavyofanyika.

Amesema, "Sababu ya sisi kuwa Incirlik ni mchango wa Ujerumani katika vita dhidi ya IS. Kuna majukumu mawili, kujaza mafuta kwenye ndege zikiwa angani na upelelezi wa ndege za Tonardo. Majukumu yote mawili ni muhimu na ni mchango wa ziasa katika muungano dhidi ya ugaidi."

Syrien-Einsatz der Bundeswehr - Tornado
Ndege aina ya Tonardo ambazo hutumika kwa upelelezi zilizoko kwenye kambi ya IncirlikPicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Ujerumani ina takriban wanajeshi 270 walioko katika kambi ya Incirlik, pamoja na ndege za upelelezi aina ya Tonardo pamoja na ndege ya mafuta. Duru zinaarifu kuwa itachukua takriban miezi miwili uhamisho huo kukamilika.

Majeshi ya Ujerumani ni sehemu ya muungano wa kimataifa dhidi kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu, IS, na viongozi wa nchi hiyo wanasema ni muhimu kwa wabunge kutembelea kambi hizo kila wanapohitaji. 

Masuala makubwa yaliyochangia kuzorota kwa mahusiano kati ya Ujerumani na Uturuki ni pamoja na Ujerumani kuwapa hifadhi ya kisiasa wanajeshi na wanadiplomasia wa Uturuki na waliokuwa wakituhumiwa na Uturuki kuwa na mahusiano na vuguvugu linaloongozwa na mhubiri wa kidini, Fethullah Gulen.

Uturuki inamtuhumu Gulen ambaye hivi anaishi nchini Marekani kwa kuandaa mapinduzi yaliyoshindwa mwezi Julai mwaka jana nchini Uturuki. Hata hivyo Gulen anapinga tuhuma hizo na hadi sasa Marekani imekataa kumkabidhi kwa Uturuki.

Lakini pia mvutano baina ya nchi hizo umetiwa chachu zaidi na masuala kama Uturuki kuwatia kizuizini waandishi wa habari wawili wa Ujerumani na kwa upande mwingine hatua ya mamlaka za ndani za Ujerumani kuzuia mikutano ya kampeni wakati wa kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba nchini Uturuki, kwa Waturuki waishio Ujerumani, ambayo ilikuwa ihutubiwe na mawaziri wa Uturuki.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE.
Mhariri:  Iddi Ssessanga