Ujerumani yamuonya Trump kuhusu Jerusalem | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yamuonya Trump kuhusu Jerusalem

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel ameionya Marekani juu ya hatari ya kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv na kuupeleka Jerusalem akisema hatua hiyo haitapunguza mgogoro uliopo.

Sigmar Gabriel ametoa onyo hilo baada ya Rais Donald Trump kusema atauhamisha ubalozi huo na kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas aliyearifiwa na Trump kuhusiana na mipango ya kuuhamisha ubalozi huo amesema hatua hiyo itasababisha madhara katika ukanda huo na duniani kwa ujumla.

Licha  ya  hatua hiyo kupingwa kwa kiwango kikubwa na Jumuiya ya kimataifa, Ikulu ya Marekani-White House imesema Rais Trump anatarajia kutoa tamko kuhusiana na suala hilo leo Jumatano.

Hata hivyo, Trump anaripotiwa kuwa atatia saini sheria itakayochelewesha hatua hiyo ya kuhamisha ubalozi kutoka Tel Aviv kwa miezi sita zaidi. Rais Mahmoud Abbas amesema  Trump alimuarifu juu ya mipango ya kuhamisha ubalozi wa Marekani, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la habari la mamlaka ya ndani ya Palestina

UN Generalversammlung in New York | Sigmar Gabriel, Außenminister Deutschland (Reuters/L. Jackson)

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel

.

Kwa mujibu wa msemaji wa ofisi ya rais wa Paletina, Nabil Abu Rudeineh, Abbas ameonya juu ya madhara yatakayotokea iwapo hatua hiyo itatekelezwa kutokana na hali halisi inayohusiana na mchakato wa kutafuta amani, usalama na uthabiti katika ukanda huo na duniani kwa ujumla.

Wapalestina wanadai Jerusalem Mashariki kama mji mkuu wa taifa lao la baadaye iwapo suluhisho la mataifa mawili linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa litakubaliwa na ambalo linatarajiwa kuhitimisha mgogoro uliodumu kwa miongo kadhaa.

Suala linalohusiana na hadhi ya mji wa Jerusalem limekuwa ni kikwazo cha muda mrefu wakati wa mazungumzo ya amani yaliyokwishafanyika kati ya Israel na Palestina hasa kuhusiana na swali ni jinsi gani wanaweza kuugawa mji huo kwa kuzingatia pia suala linalohusu maeneo matakatifu.

Jumuiya ya kimataifa haijawahi kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel 

USA Präsident Donald Trump (Reuters/J. L. Duggan)

Rais wa Marekani Donald Trump

Jumuiya ya kimataifa haijawahi kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel au hatua ya Israel kuyatwaa maeneo ya mashariki ya mji huo wakati wa vita ya mwaka 1967 iliyodumu kwa siku sita.

Hata hivyo Maafisa wa Israel wamekuwa wakiushawishi utawala wa Rais Donald Trump kufanya hivyo.

Waziri wa ulinzi wa Israel, Avigdor Lieberman ametoa mwito kwa ikulu ya Marekani kutumia nafasi hii ya kihistoria  kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel akisema ana matumaini ya kuona ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem wiki ijayo au mwezi ujao.

Barani Ulaya mpango huo wa Marekani umepokewa kwa mashaka pamoja na maonyo. Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amemkumbusha Trump kuwa hadhi ya Jerusalem itapaswa kuamriwa wakati wa mazungumzo kujadili suluhisho la mataifa mawili.

Ama kwa upande mwingine mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini amesema suala lolote linaloonekana kukwamisha juhudi za kuanzisha mazungumzo ya amani halipaswi kuungwa mkono. Moghereni ameyasema hayo hapo jana baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson.

Mwandishi: Isaac Gamba /DW/AP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com