Ujerumani yaionya Israel kuhusu ujenzi wa makaazi ya walowezi | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yaionya Israel kuhusu ujenzi wa makaazi ya walowezi

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema ujenzi wa makaazi ya walowezi unaoendelezwa na Israel unahujumu mazungumzo ya kutafuta amani Mashariki ya kati.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani alikuwa Israel jana kwa ziara ya siku moja ili kuzungumzia mchakato wa kupatikana suluhu ya amani kwa mzozo wa muda mrefu wa mashariki ya kati siku ambayo ilitawaliwa zaidi na mazishi ya aliyekuwa waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon.

Steinmeier alikutana na mpatanishi mkuu wa Israel Tzipi Livni kisha kuhudhuria mazishi ya Sharon kabla ya kusafiri hadi Ramallah kukutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmud Abbas.

Ujenzi usiwe kikwazo

Akizungumza na waandishi habari baada ya kukutana na Abbas,Steinmeier alisema mazungumzo yanayoendelea kati ya Palestina na Israel yaliyofufuliwa mwezi Julai mwaka jana, hayapaswi kutatizwa na matangazo ya kila mara kutoka Israel ya kujenga makaazi mapya ya walowezi katika ukingo wa magharibi na mashariki mwa Jerusalem.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Wiki iliyopita, siku chache tu baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kuzuru Mashariki ya kati ili kupiga jeki mchakato wa kupatikana amani,Israel ilitangaza mipango ya kujenga makaazi mapya 1800 na kuzua shutuma kali kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya.

Steinmeier amesema wakati ni sasa kwa pande zote mbili kujizatiti ili ipatikane suluhu la kudumu.

Mpatanishi mkuu wa Palestina Saeb Erakat amesema nchi yake inafanya kila iwezalo kufanikisha mchakato huo wa amani na kuitaka Ujerumani na umoja wa Ulaya kuishinikiza Israel kuhusu ujenzi huo tete.

Sehemu ya makaazi ya walowezi yanayojengwa na Israel

Sehemu ya makaazi ya walowezi yanayojengwa na Israel

Ujerumani imekuwa ikichukulika mshirika wa karibu wa Israel kutoka bara Ulaya tangu kukamilika kwa vita vikuu vya pili vya dunia lakini katika kipindi cha hivi karibuni imekuwa kitoa shinikizo kwa waziri mkuu wa isreal Benjamin Netanyahu kujizuia kuendelea na ujenzi katika maeneo yanayozozaniwa ya Palestina ili kutotatiza juhudi za kutafuta amani Mashariki ya kati zinazoongozwa na Marekani.

Baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Palestina,Steinmeier alirejea Jerusalem alikoandaliwa dhifa ya chakula cha jioni na mwenzake wa Israel Avigdor Lieberman na baadae kurejea Ujerumani.

Mwezi ujao Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajiwa kwenda Israel kujibu mualiko wa waziri mkuu Benjamin Netanyahu na kushiriki katika mazungumzo ya pamoja kati seikali hizo mbili.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa
Mhariri: Hamidou Oummilkheir

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com