Ujerumani yaidhinisha Mkataba wa Lisbon | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.09.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yaidhinisha Mkataba wa Lisbon

Mkataba huo wa Umoja wa Ulaya umetiwa saini na Rais wa Ujerumani, Horst koehler.

default

Rais Horst Koehler wa Ujerumani (Shoto) na Rais Gjorge Ivanov wa Macedonia (Kulia).

Ujerumani imeidhinisha Mkataba wa Umoja wa Ulaya unaojulikana kama Mkataba wa Lisbon, hivyo kuziacha nchi tatu za umoja huo kuuidhinisha mkataba huo ili kuufanya Umoja wa Ulaya kutekeleza majukumu yake kirahisi. Mkataba huo umesainiwa leo na Rais Horst Koehler, ikiwa ni hatua ya mwisho iliyokuwa inangojewa kwa ajili ya idhinisho hilo. Hatua ya Rais Koehler kusaini Mkataba huo wa Lisbon, inazifanya nchi tatu za Ireland, Poland na Jamhuri ya Czech zikiwa bado hazijauidhinisha mkataba huo unaohitajika kupitishwa kwa pamoja. Ujerumani imefikia uamuzi wa kuidhinisha mkataba huo baada ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo mwezi Juni, mwaka huu, kutaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho ili mkataba huo kuidhinishwa. Msemaji wa Rais koehler, amesema idhinisho la mwisho la Ujerumani litafanyika wiki hii, baada ya sheria kuchapishwa katika gazeti la kiserikali na Rais Koehler kusaini nyaraka rasmi Ijumaa hii, ili iweze kuwasilishwa kwa maafisa wa mkataba huo mjini Roma.

Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameelezea kufurahishwa kwake na hatua iliyochukuliwa na Rais Koehler ya kuidhinisha mkataba huo. Akizungumza na Radio ya mkoa wa Bavaria, Bibi Merkel amesema hatua hiyo ni mafanikio makubwa na amewapongeza wabunge wa ujerumani kwa kuidhinisha sheria itakayowaruhusu kuuridhia mkataba huo wa Lisbon, japokuwa wanakabiliwa na kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika siku ya Jumapili.

Ijumaa iliyopita, Baraza la mabunge ya mikoa nchini Ujerumani-Bundesrat, liliidhinisha sheria hiyo itakayowaruhusu wabunge kuuridhia mkataba huo wa Lisbon na tayari bunge la Ujerumani-Bundestag lilishaidhinisha sheria hiyo. Kwa mujibu wa sheria hiyo mpya, Bundesrat na Bundestag lazima zipewe taarifa kama mabadiliko yanafanyika kwa mfano katika haki ya kura ya Veto ya Ujerumani na lazima litaarifiwe mapema kuhusu mapendekezo ya utungaji wa sheria za Umoja wa Ulaya.

Mkataba huo wa Lisbon umeandaliwa kwa kuchukua nafasi ya mkataba wa sasa wa Nice, ulioanzishwa wakati Umoja wa Ulaya ukiwa na nusu ya idadi ya wanachama walioko sasa. Endapo utaanza kutumika rasmi, Umoja wa Ulaya utaachana na mfumo wake wa kupokezana urais na watachagua kiongozi kwa muda maalum.

Ireland ambayo iliingiza Umoja wa Ulaya katika matatizo kwa kukataa mkataba huo katika upigaji kura za maoni mwaka uliopita, imepanga kufanya uchaguzi wake wa pili wa kura ya maoni Oktoba Pili, mwaka huu na kura zinaonyesha wapiga kura wa nchi hiyo mara hii watapiga kura ya ndiyo. Mabunge ya mataifa mengi yameidhinisha mkataba huo wa Lisbon bila kufanya mageuzi yoyote.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/DPAE)

Mhariri: Mwadzaya Thelma

 • Tarehe 23.09.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JnTn
 • Tarehe 23.09.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JnTn
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com