Ujerumani yaamini siasa za nje za Marekani hazitabadilika | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yaamini siasa za nje za Marekani hazitabadilika

Hata baada ya chama cha Rais Barack Obama cha Democrats kupoteza udhibiti wa Baraza la Wawakilishi kufuatia uchaguzi wa juzi (2 Novemba 2010), Ujerumani inaamini kwamba mahusiano ya Marekani na Ulaya hayatabadilika

Rais Barack Obama wa Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani

Uchaguzi wa Jumanne (2 Novemba 2010) umekiwacha chama kinachotawala cha Democrat kikiwa kimepoteza wingi wake kwenye Baraza la Wawakilishi, ingawa chama hicho cha Rais Barack Obama kimeendelea kushikilia hatamu ya Baraza la Seneti.

Maoni ya mwenyewe Rais Obama kuhusu uchaguzi huu ni kwamba Wamarekani wanavitaka vyama vya Democrtas na Republican kushirikiana kutafuta suluhisho kwa changamoto inayolikabili taifa la Marekani hivi sasa.

Lakini nchini Ujerumani kuna maoni tafauti. Kuna wengine wanaoona kuwa hii ni hasara kwa Obama, wengine wanaona ni kura dhidi ya Democrats, lakini sio kura kwa ajili ya Republicans.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle

Waziri wa Mambo ya Nje, Guido Westerwelle, anasema kwamba hatarajii kuwa matokeo haya ya uchaguzi yataathiri siasa za nje za Marekani. Marekani ina uhusiano na mataifa ya Ulaya ya Magharibi, ikiwemo Ujerumani.

Hata Mratibu wa serikali ya Shirikisho la Ujerumani anayehusika na masuala ya Ushirikiano na Marekani, Hans-Ulrich Klose, ambaye anatokea chama cha Social Democrat, anaamini kwamba siasa ya nje ya Marekani itabakia kuwa ile ile. Lakini siasa za ndani, bila ya shaka, ndizo hasa zitakazoathirika.

"Lililo la uhakika ni kwamba siasa za ndani za Obama zitabadilishwa. Hata hivyo, hilo linaweza likawa na faida zake. Maana Repubican wamepata wingi kwenye Baraza la Wawakilishi tu, na watakapotaka kulipinga kila jambo kutoka serikalini kwa maslahi ya kupinga tu, kama chama watajikuta wanakosa thamani, na hilo ni tatizo kubwa kwa Marekani." Anasema Klose.

Katika hali ambapo vyama viwili vinashikilia mihimili tafauti ya dola, Republicans wanashika Baraza la Kutunga Sheria na Democrats wanashika Ikulu, inakuwa si jambo rahisi kupata muafaka kama ilivyo hapa Ujerumani. Tayari kwa miaka hii miwili ya utawala wa Obama, vyama hivyo vimeshaoneshana kupingana sana kwenye mabaraza ya sheria, kiasi ambacho sasa inatisha kufikiria watakavyoweza kufanya kazi pamoja.

Kushindwa kwa Obama ni muakisiko wa kutokuridhika na kuvunjika moyo walikonako wapiga kura wa Marekani dhidi ya hali ngumu ya maisha. Kupanda kwa kiwango cha wasio na ajira na kuporomoka kwa biashara yatakuwa mambo yatakayotawala mabishano kati ya Congerss na Ikulu hadi uchaguzi ujao wa Rais.

Kuhusu muendelezo wa mahusiano ya Trans Antlantik, mwanasiasa wa kiliberali Rainer Stinner anaona kwamba, kwa ujumla Baraza la Wawakilishi la Marekani litapitisha maamuzi ya kuongeza sera za udhibiti na umiliki mkubwa wa hali ya uchumi katika eneo hili.

Ambapo Mratibu wa Mahusiano ya Trans-Antantik, Hans-Ulrich Klose, anaamini kwamba siasa za nje za Obama hazitaguswa na matokeo ya uchaguzi huu, mbunge Ruprecht Polenz wa chama cha Chrisitan Democratic anaamini kwamba hali inaweza kuwa tafauti.

"Tumekuwa tukishuhudia matatizo na migogoro ikipelekea ufumbuzi hapa duniani, lakini pia ikitegemeana. Ikiwa Wamarekani hawako imara, maana yake ni kwamba hapa Ulaya tunalazimika kufanya mengi kuhusu hilo, maana hali zinaathiriana. Hatuna muda wa kutosha, bali tunahitaji sasa kujiimarisha.“ Anasema Polenz.

Yote kwa yote, siasa za Marekani na Ulaya zina mengi baina yao. Na Ujerumani, kikiwa kitovu cha Bara la Ulaya, ina mengi zaidi yanayoikutanisha na Marekani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Fuchs, Richard/ZPR

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

 • Tarehe 04.11.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Pxwl
 • Tarehe 04.11.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Pxwl

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com