1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Ufaransa na Ureno Kundi moja Euro 2020

Bruce Amani
1 Desemba 2019

Washindi wa Kombe la Dunia Ufaransa, mabingwa wa sasa wa Ulaya Ureno na Ujerumani wamepangwa katika Kundi moja gumu la F katika michuano ya Euro 2020

https://p.dw.com/p/3U24S
Rumänien Bukarest | Auslosung Fußball-EM 2020 | Deutschland, Bundestrainer Joachim Löw
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Ujerumani ya Joachim Loew iliorodheshwa ya kwanza katika droo ya Jumamosi mjini Bucharest lakini wakapewa kibarua kikali kutoka kibakuli cha pili dhidi ya mabingwa wa dunia na Ureno kutoka kibakuli cha tatu. Mshindi wa mechi za mchujo atakamilisha kundi hilo.

Italia yake Roberto Mancini itafungua mashindano hayo kwa mechi ya Kundi A dhidi ya Uturuki mjini Rome mnamo Juni 12 kabla ya kukabiliana na Uswisi na Wales.

England itakutana na Jamhuri ya Czech na katika mchuano wa marudio ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018, Croatia katika Kundi D wakati Uhispania ikivaaana na Poland na Sweden katika Kundi gumu la E.

Finland, timu pekee iliyodhibitishwa kushiriki kwa mara ya kwanza, itaungana na Ubelgiji, Urusi na Denmark katika Kundi B. Ukraine na Uholanzi zinaungana na Austria katika Kundi C.

Hili ni Kundi la Kifo

Ujerumani angalau wanaweza kujiliwaza kwa kuwa watacheza mechi zao zote mjini Munich. "Hili ni kundi la kifo,” alisema Loew. "kwa timu yetu changa, hii itakuwa changamoto kubwa sana lakini pia motisha kubwa."

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps aliliita "kundi gumu kabisa kati ya yote sita," lakini akaongeza kuwa Ujerumani na Ureno "hazitakuwa na furaha pia kuwa na Ufaransa katika kundi lao."

Timu mbili pekee za kwanza kwenye kila kundi zina nafasi ya kusonga mbele lakini Kundi F huenda likamtoa mmoja kati ya timu nne bora za nafasi ya tatu.

Kama Hungary, Bulgaria au Iceland zitapenya kupitia njia ya mchujo, zitajiunga na miamba hao watatu. Kama Romania itapenya badala yake itajiunga na Kundi C ambalo wako pamoja na Uholanzi, na kuacha moja kati ya Georgia, Macedonia Kaskazini, Belarus au Kosovo katika Kundi F.

Mechi ya kwanza kati ya 51 za mashindano hayo itakuwa mjini Rome, ambako Italia, italenga kuweka mwanzo mzuri dhidi ya Uturuki.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Sekione Kitojo