1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Uturuki kuujadili mzozo wa wakimbizi

Caro Robi22 Januari 2016

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ataishinikiza Uturuki kuzidisha juhudi zake za kukabiliana na mmiminiko wa wakimbizi barani Ulaya wakati atapofanya mkutano leo na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/1Hi8C
Picha: Reuters/E. Vidal

Ujerumani na Uturuki zimeibuka kuwa wahusika wakuu katika kushughulikia mzozo wa wahamiaji ambao ndiyo mkubwa zaidi kuwahi kulikumba bara hilo tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia na nchi zote mbili zitajaribu kulizungumzia kwa kina suala hilo wakati mabaraza yao ya mawaziri yatakapokutana leo mjini Berlin.

Mkutano huo kati ya Uturuki na Ujerumani unakuja baada ya mashambulizi ya kigadii yaliyotokea mjini Istanbul wiki iliyopita ambapo raia kumi wa Ujerumani waliuawa.

Msemaji wa Merkel, Steffen Seibert amesema mazungumzo pia yataangazia kampeini ya kimataifa ya kupambana dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu IS.

Ushirikiano ni muhimu

Hapo jana, akihutubu katika jukwaa la kiuchumi la Dunia la Davos, Davutoglu alisema kuna haja ya kuwepo ushirikiano kati ya wahusika waku katika kutatua tatizo la wahamiaji na kitisho cha ugaidi.

Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu
Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet DavutogluPicha: Reuters/M. Sezer

Matokeo ya mkutano wa leo sio tu muhimu kwa Merkel ambaye anakabiliwa na shinikizo kubwa nchini Ujerumani kutokana na sera yake ya kuwapokea maelfu ya wahamiaji lakini pia matokeo ya mkutano huo yanasubiriwa kote Ulaya ambako maoni ya umma yanazidi kuwa hasi dhidi ya wahamiaji ambao wanaongezeka kila uchao.

Kansela huyo ya Ujerumani ameahidi kuchukua hatua madhubuti kupunguza ongezeko la wakimbizi baada ya wahamiaji milioni moja na laki moja kuingia Ujerumani mwaka jana.

Uturuki ina wajibu muhimu katika kuusaidia Umoja wa Ulaya kukabiliana na wimbi hilo la wakimbizi kwasababu wengi wa wahamiaji hao huwasili kwanza Uturuki kabla ya kuendelea na safari kuelekea nchi za Umoja wa Ulaya.

Merkel atamuomba Davutoglu kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya mwezi Novemba ambapo Umoja huo uliipa Uturuki mamilioni ya fedha kuisaidia kushughulikia tatizo hilo.

Licha ya makubaliano hayo, wakimbizi kati ya 2,000 na 3,000 wanawasili kila siku Ugiriki wakitokea Uturuki. Umoja wa Ulaya haujaweza kutimiza wajibu wao wa makubaliano kwasababu nchi wanachama bado wanavutana kuhusu ni kiasi gani kila nchi inapaswa kulipa kama sehemu ya msaada kwa wakimbizi milioni 2.2 wa Syria wanaoishi Uturuki.

Obama aahidi kumsaidia Merkel kushughulikia wakimbizi

Gazeti la Die Welt limeripoti kuwa kuna uwezekano Ujerumani ikaahidi msaada zaidi wa kifedha kwa Uturuki. Hapo jana Merkel alizungumza na Rais wa Marekani Barack Obama kwa njia ya simu kuhusu suala hilo la wakimbizi. Obama aliahidi kile kilichoelezwa kuwa msaada wa kutosha katika kukabiliana na mzozo wa wakimbizi.

Rais wa Marekani Barack Obama na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Rais wa Marekani Barack Obama na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa

Viongozi hao wawili walikubaliana kuwa suluhisho pekee la kuvimaliza vita vya Syria ni la kisiasa na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika kushughulikia masuala ya Syria na ya nchi jirani.

Merkel anatarajiwa kuwa mwenyekiti mwenza wa mkutano wa wafadhili kuchangisha fedha za kuwasaidia Wasyria. Mkutano huo utaandaliwa tarahe nne mwezi ujao mjini London, Uingereza.

Wanasiasa waliokutana Davos katika jukwaa la kiuchumi la dunia wameonya Umoja wa Ulaya huenda ukasambaratika iwapo hakutakua na mtazamo wa pamoja wa kushughulikia mzozo wa wakimbizi na changamoto za kiusalama.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga