1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Ufaransa kutia saini mkataba wa ushirikiano

Sekione Kitojo
22 Januari 2019

Kansela wa Ujerumani  Angela Merkel  na  rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanatarajiwa kutia  saini mkataba mpya wa urafiki baina ya nchi zao, katika  mji wa magharibi nchini Ujerumani wa Aachen Jumanne(22.01.2019).

https://p.dw.com/p/3BwzI
Belgien, EU-Gipfel - Emmanuel Macron, Präsident von Frankreich und Bundeskanzlerin Angela Merkel
Picha: AFP/Getty Images

Utiaji  saini  mkataba  huo  unajiri  mnamo wakati wa maadhimisho  ya  miaka  56 ya  kutiwa  saini  kwa  makubaliano  ya  Elysee  mjini  Paris.

Deutschland Berlin Macron und Merkel im Bundestag
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto) na kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kulia)Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Sohn

Mkataba  huo  wa  Aachen  unaziweka  nchi  hizo  mbili jirani  katika  dhamira  ya  kuimarisha  ushirikiano  wao katika  sera  za  Umoja  wa  Ulaya  na  kufanyakazi kuelekea  katika  sera  ya  pamoja  ya  mambo  ya  kigeni na usalama.  Kufanyakazi  kwa  pamoja  katika  masuala ya  kiuchumi  pia  kutaimarishwa. Mkataba  huo  utahitaji kuidhinishwa  na  mabunge  ya  nchi  zote  kabla  ya utekelezaji  wake.

Katika  mahojiano  na  vyombo  vya  habari  kabla  ya mkutano  huo,  mwanasiasa  mkongwe  wa  Ujerumani kutoka  chama  cha  Christian Democratic  Union  CDU Wolfgang Schaeuble, ambaye  kwa  sasa  ni  spika  wa bunge  la  Ujerumani Bundestag,  ametoa  wito  wa  kuwa na  malengo  mapana  ya  sera  za  Umoja  wa  Ulaya.

Ushirikiano wa  karibu  unahitajika

Amesema kwa  mara  nyingine Ujerumani na Ufaransa zinahitaji  miradi ya  maana  na  dhabiti  ya ujumuisho ambayo  inaweka  wazi  kwa  wananchi  kwamba  Ulaya inafanikisha  mambo  katika  kiwango  tofauti  kabisa  na ubora  kuliko  kila  nchi  pekee yake.

Deutsch-Französischer Freundschaftsvertrag
Sanamu lililoko katika mji wa magharibi nchini Ujerumani wa Aachen likiwa katikati ya bendera za Ujerumani na UfaransaPicha: picture alliance/dpa/F. Gambarini

Katika  uhariri  ulioandikwa  katika  gazeti  la  Neue Presse leo,  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Ujerumani Heiko Maas  ametoa  wito  wa  ushirikiano  wa  karibu  baina  ya Ufaransa  na  Ujerumani  mnamo  wakati  ambapo  siasa kali  za  mrengo  wa  kulia  zinaongezeka, kuna mifarakano ya  kibiashara  na  mizozo  inaliathiri bara  la  Ulaya.

Amesema hakupaswi kuwepo hali ya kubweteka, na kuongeza kuwa uhusiano  imara  wa  Ufaransa  na Ujerumani, unahitaji  kutekelezwa ili  kuwezesha kuhudumia  Ulaya  iliyo  imara  na  yenye  uwezo.

Chama  cha  Social  Democratic SPD, chama kinachoshiriki  katika  kuunda  serikali  ya  muungano mkuu  unaoongozwa  na  kansela  Merkel, pia  kimetoa wito  wa  uharaka  wa  utekelezaji  huo.

Mbunge mwandamizi kutoka chama hicho Achim Post amesema kwa muda  mrefu  sana, kansela  Merkel hususan  amesababisha  juhudi  za  Ulaya  kutoka  kwa rais  wa  Ufaransa  kuyeyuka.

Mkataba  wa  Elysee

Januari 22, mwaka  1963, rais  wa  Ufaransa Charles de Gaulle  na  kansela  wa  kwanza  wa  Ujerumani  baada  ya vita  Konrad Adenauer walitia  saini  mkataba  wa  Elysee ambao uliweka  njia  ya  mashauriano  ya  kila  mara  kati ya  mahasimu  hao  wa  zamani  katika  ngazi  ya  juu  ya serikali.

Frankreich Gelbwesten | Protest in Paris
Maandamano ya "vizibao vya njano" nchini UfaransaPicha: Getty Images/AFP/P. Lopez

Nchi  hizo  mbili  hivi  sasa  zinasogea  katika  kuimarisha uhusiano  wao  wakati  ambapo  Umoja  wa  Ulaya  uko katika  hali  ya   mkanganyiko.

Talaka baina  ya  Umoja  huo  na  Uingereza, maarufu kama  Brexit  inakaribia. Merkel, kansela  wa  Ujerumani tangu  mwaka  2005, ameamua  kuachana  na  uongozi  wa chama  chake  cha CDU na  hatagombea  tena  uchaguzi ujao.

Na  Macron  anakabiliwa  na  wiki  kadhaa  za maandamano  ya  kile  kinachojulikana  kama , "maandamano  ya  vizibao  vya  manjano"  kutokana  na kupanda  kwa  gharama  za  maisha pamoja  na  kodi nchini  Ufaransa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae

Mhariri: Daniel Gakuba