1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Israel zaadhimisha miaka 50 ya mauaji ya Munich

Amina Mjahid
5 Septemba 2022

Marais wa Ujerumani na Israel wameongoza hafla ya kumbukumbu ya miaka 50 tangu yalipotokea mauaji wakati wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 1972 mjini Munich.

https://p.dw.com/p/4GRn6
Gedenkveranstaltung zum 50. Jahrestag des Olympiaattentats
Picha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Marais hao wana matumaini kwamba makubaliano yaliosubiriwa kwa muda mrefu ya ulipaji fidia kwa familia za wahanga, itawasaidia kuanza kupona polepole kutokana na visa vilivyojaa huzuni. Mvutano kuhusu pendekezo la fidia kwa familia ya wahanga lililotolewa na serikali ya Ujerumani ulitishia kuvuruga hafla hiyo, kwa familia ya wahanga kususia kuhudhuria.

Lakini hatimae makubaliano yalifikiwa siku ya Jumatano, na Ujerumani iliridhia kutoa yuro milioni 28 kama fidia. Katika makubaliano hayo Ujerumani kwa mara ya kwanza pia ilikubali kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha usalama wa wanariadha wa Israel, hali iliyopelekea kuuwawa kwa wanariadha hao 11, mikononi mwa wanamgambo wa kipalestina wa kundi la Black September.

Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier alikiri jana Jumapili kwamba ni aibu kwa Ujerumani kuchukua muda mrefu kufikia makubaliano na familia za wahanga huku akisema taifa lake limejikokota kutambua machungu yaliyopitiwa na familia hizo.

Maafisa Ujerumani wasema wakati wa kuomba msamaha umefika

Staatsbesuch des Präsidenten von Israel in Deutschland
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na mwenzake wa Israel Isaac Herzog katika kumbukumbu ya miaka 50 tangu mauaji ya MunichPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Akizungumza na gazeti la Funke, afisa mmoja wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya kupambana na chuki dhidi ya wayahudi Felix Klein, amesema muda umefika kwa Ujerumani kuomba msamaha akisema anatumai rais Steinmeier atapata maneno sahihi ya kusema wakati wa hafla hiyo. 

Tarehe 5 mwezi Septemba mwaka 1972 wanaume wanane waliojihami kwa silaha wanaoaminika kuwa wanamgambo wakipalestina waliivamia timu ya wanariadha wa Israel  katika michezo ya olimpiki yaliyofanyika wakati huwa na kuwapiga risasi na kuwaua wanariadha wawili na kuwachukua mateka wengine 9.

Miaka 50 tangu shambulizi kwenye michezo ya Olimpiki mjini Munich

Polisi Magharibi mwa Ujerumani walizembea katika operesheni ya kuwaokoa waliochukuliwa mateka na baadae wote tisa waliuwawa, afisa mmoja wa polisi na wanamgambo watano kati ya wanane waliokuwepo. Michezo hiyo ya olimpiki ilikuwa na nia ya kuonesha Ujerumani  mpya baada ya miaka 27 ya mauaji ya wayahudi lakini badala yake ilifungua ukurasa mpya na mvutano mkubwa zaidi na Israel.

Aidha rais wa Israel Isaac Herzog ameelezea matumaini yake kwamba makubaliano yaliyofikiwa yatasaidia kuondoa familia za wahanga katika machungu na kuanza pole pole kupona akionggeza kuwa kuanzia leo watu wataendelea kukumbuka na kukemea na kujifunza kutokana na visa viovu vilivyotokea siku za nyuma.

Hapo kesho Jumanne Herzog anatarajiwa kulihutubia bunge la Ujerumani Bundestag na kutembelea kambi ya wanazi ya Bergen Belsen ambako babake na pia rais wa zamani wa Israel Chaim Herzog waliorodheshwa miongoni mwa wakombozi mwaka 1945.

Chanzo: afp