1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Muuguzi aliyeuwa wagonjwa 85 afungwa maisha

Daniel Gakuba
6 Juni 2019

Mahakama nchini Ujerumani imemhukumu kifungo cha maisha, muuguzi wa hospitali aliyepatikana na hatia ya kuwauwa makusudi wagonjwa 85 waliokuwa chini ya uangalizi wake, kwa kuwasababishia mshituko wa moyo.

https://p.dw.com/p/3JxcP
Deutschland Prozess gegen Patientenmörder Högel
Niels Hoegel aliyepatikana na hatia ya kuuwa wagonjwa 85Picha: picture-alliance/dpa/H.-C. Dittrich

Mahakama ya mji wa Oldenburg Kaskazini mwa Ujerumani imemkuta na hatia muuguzi huyo, Niels Hoegel mwenye umri wa miaka 42, ya kuwauwa wagonjwa wake kwa kuwachoma sindano ya sumu kati ya mwaka 2000 na 2005 alipofumwa akifanya uhalifu huo. Tayari ameishi gerezani kwa miaka  miaka 10 kwa hatia nyingine ya mauaji ya watu sita.

Polisi wanashuku kuwa huenda Hoegel aliangamiza maisha ya wagonjwa zaidi ya 200. Waendeshamashitaka walilazimika kuifukua miili ya watu 130 katika kukusanya ushahidi.

Mahakama haikuweza kuthibitisha idadi kamili ya wahanga wa mtu huyo, kwa sababu miili ya marehemu wengi ilichomwa moto kabla ya kufanyiwa uchunguzi.

Uovu usioeleweka kwa akili ya binadamu

Prozess gegen Krankenpfleger Niels Högel
Hoegel alifanya kazi katika hospitali hii ya OldenburgPicha: picture-alliance/dpa/H.-C. Dittrich

Jaji wa mahakama ya Oldenburg, Sebastian Buehrmann amesema ni vigumu kuelewa sababu ya mlolongo huo wa mauaji, ambayo amesema yamepitiliza kile ambacho binadamu anaweza kukielewa.

Jaji Buehrmann vile vile ameomba radhi kwa familia za wahanga, kwa sababu mahakama haikuweza kupata majibu kwa masuala yote yanayoulizwa kuhusu uovu huo.

Mnamo siku ya mwisho ya kusikilizwa kesi dhidi yake, muuaji huyo, Niels Hoegel ameomba msamaha kwa matendo yake aliyokiri kuwa ni ya kutisha.

Hoegel alikamatwa mwaka 2005 baada ya kufumwa akimdunga mgonjwa sindano yenye dawa ambayo hakuandikiwa na daktari, na mwaka 2008 alihukumiwa kifungo cha miaka saba kwa hatia ya kujaribu kuuwa.

Asema alifurahia kuwapa wagonjwa mshituko wa moyo

Deutschland Prozess gegen Patientenmörder Högel
Vyombo vya habari vilifuatilia kesi hiyo kwa karibuPicha: picture-alliance/dpa/H.-C. Dittrich

Katika kesi hiyo ya kwanza, Hoegel alisema alifurahia kitendo cha kusimamisha kwa makusudi mapigo ya moyo wa mgonjwa, na kisha kuanza utaratibu wa kumpa huduma ya kuyaanzisha tena. Wagonjwa wote aliowaweka katika matatizo hayo walikufa.

Kutokana na shinikizo la familia za wahanga, kesi ya pili dhidi yake iliendeshwa kati ya mwaka 2014-2015, ambapo alipatikana na hatia nyingine ya kuuwa watu watano na kupewa hukumu ya kifungo cha miaka 15 jela, ambayo nchini Ujerumani inajulikana kama kifungo cha maisha.

Na awamu ya tatu kesi yake ilifuatia kuanzia Oktoba mwaka jana, ambapo Jaji Buehrmann alisema lengo lilikuwa kuweka uwazi katika upeo wa mauaji hayo yaliyoruhusiwa kuendelea kwa miaka kadhaa bila kusimamishwa.

Jaji huyo aliilinganisha kesi hiyo na nyumba yenye vyumba vya giza, akisema mahakama inataka kuweka nuru katika vyumba hivyo.

 

ape, afpe