1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Mradi wa umeme wa Tanzania wapigiwa kura bungeni

Zainab Aziz
18 Januari 2019

Bunge la Ujerumani limepitisha mswada wa kuitaka serikali ya Ujerumani itafute njia mbadala ya mradi wa Tanzania wa kuzalisha nishati ya umeme kwenye  bonde  la Stiegler ili  kulinda turathi na asili.

https://p.dw.com/p/3BlZt
Berlin Reichstag
Picha: picture-alliance/NurPhoto/A. Widak

Vyama vilivyomo katika serikali ya mseto ya Ujerumani vimeitaka serikali itafute njia nyingine badala ya ile ya mradi wa kuzalisha nishati ya umeme kwenye bonde la Stiegler kwenye mto rufiji kusini mwa Tanzania Wabunge wa vyama vya CDU/CSU, Kijani na AFD walishiriki katika kupiga kura hiyo lakini chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD, hakikushiriki. Azimio la vyama vya CDU,CSU na SPD pia linatokana na mapendekezo ya kamati ya serikali ya Ujerumani ya ushirikiano wa kiuchumi.

Azimio lililopitishwa bungeni na vyama hiyvo vilivyomo katika serikali ya mseto ya Ujerumani linaitaka serikali kuu isaidie katika masuluhisho ya kukidhi mahitaji ya nishati ya Tanzania bila ya kuathiri mazingira. Katika azimio lao vyama hivyo vimesema mradi huo mkubwa wa kuzalisha nishati ya umeme utavuruga mfumo wa mto mmojawapo mkubwa barani Afrika.

Tanzania inakusudia kujenga bwawa kubwa la kuzalisha nishati ya umeme kwa kutumia nguvu ya maji kutoka kwenye mto rufiji.  Sehemu hiyo ni muhimu kwa shughuli za kilimo za wakaazi. Ikiwa mradi huo utaendelea  mbele bonde la Stiegler ambalo limewekwa miongoni mwa turathi za shirika la Umoja wa mataifa la UNESCO litapoteza hadhi yake na huenda likasababisha athari kubwa katika raslimali zilizopo kwenye sehemu hiyo.

Hifadhi ya wanyama pori ya Selous nchini Tanzania
Hifadhi ya wanyama pori ya Selous nchini TanzaniaPicha: Irene Quaile

Katika ombi lao kwa serikali ya Ujerumani wabunge wa vyama vya CDU,CSU na SPD wamesema sehemu  hiyo ya mbuga ya wanyama ya Selous nchini Tanzania ni eneo kubwa kabisa na kongwe la hifadhi ya wanyama pori barani Afrika.

Wabunge hao wamesema mradi huo wa bwawa la nishati utahitaji sehemu kubwa sana itakayotokana na  kukatwa kwa miti na hivyo kusababisha athari kubwa katika mazingira, tabia nchi na katika uchumi.

Wabunge wa chama cha upinzani cha FDP wameshauri kujengwa kinu cha nishati kutokana na gesi kwa  sababu Tanzania inayo gesi ya kutosha iliyogunduliwa hivi karibuni. Chama hicho cha upinzani cha FDP  kilichopinga azimio hilo kimeitaka serikali ya Ujerumani ifanye mazungumzo na serikali ya Tanzania.

Mwandishi/Zainab Aziz/Daniel Pelz/DW Berlin

Mhariri: Yusuf Saumu