1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kutuma wanajeshi kupambana na Ebola

25 Septemba 2014

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen ametangaza kuwa zaidi ya wanajeshi elfu mbili wa Ujerumani wamejitolea kwenda magharibi mwa Afrika kusaidia katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa Ebola

https://p.dw.com/p/1DKkW
Picha: DW/A. Grunau

Von der Leyen amesema aliduwaa na jinsi wanajeshi na raia walivoitikia wito aliotoa siku mbili zilizopita za kuwasaidia waathiriwa wa Ebola. Ujerumani imesema bado itafanya utaratibu wa kubaini iwapo waliojitolea wamepata chanjo zinazohitajika na wataweza kusaidia vipi kitaalamu.

Afisa wa umoja wa Ulaya Marcus Cornaro ameonya kuwa mkurupuko wa Ebola nchini Liberia unasambaa kwa kasi sana kiasi cha kwamba kunahitaji mpango mbadala kukabiliana na janga hilo nchini humo mbali na kuanzisha vituo vya kutoa matibabu.

Cornaro amesema kuna umuhimu wa kutolewa hudumua katika nyanja ya jamii kwa kuwapa mafunzo na vifaa vya kujikinga jamaa za waathiriwa ili waweze kuwahudumia wagonjwa na kujua kuwa anapokufa mwili wake haupaswi kushikwa na mtu mwinginge mbali na jamaa mmoja tu aliye na kinga.

Juhudi zaidi zinahitajika

Akizungumza katika mkutano mkuu wa umoja wa Mataifa mjini New York Marekani,Rais wa Marekani Barrack Obama ameomba kupanuliwa kwa juhudi za kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola ambao umeziathiri nchi kadhaa magharibi mwa Afrika.

Afisa wa Umoja wa Ulaya Marcus Cornaro
Afisa wa Umoja wa Ulaya Marcus CornaroPicha: DW/B. Riegert

Katika mkutano huo huo, Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan pia ametangaza kuwa nchi yake haiko tena katika hatari ya janga hilo la Ebola. Madaktari awali walisema itawabidi wasubiri kidogo kabla ya kutangaza kuwa hakuna kitisho cha Ebola Nigeria.

Hakuna visa vipya ambavyo vimeripotiwa nchini humo tangu tarehe nane mwezi huu na iwapo hakutakuwa na visa vipya, WHO imesema itatangaza rasmi tarehe 20 mwezi ujao kuwa Nigeria haina Ebola.

Wakati huo huo, mkuu wa kituo cha matibabu cha Liberia amewahimiza wahanga wa Ebola kujitolea kutoa damu ili itumike kuwatibu wagonjwa wa Ebola. Daktari Attai Omoruto kutoka Uganda ambaye anasimamia kituo kipya cha matibabu mjini Monrovia amesema wanahitaji wahanga kujitokeza na kusaidia kwa kutoa damu.

Damu ya wahanga kusaidia kutibu

Tafiti zinadokeza kuwa damu kutoka kwa wahanga wa Ebola huenda ikazuia au kutibu ugonjwa wa Ebola kwa wengine. WHO mapema mwezi huu ilisema chembechembe kutoka damu za wahanga zinaweza kusaidia katika matibabu ya Ebola.

Maafisa wa afya wakiubeba mwili wa aliyekufa kwa Ebola Liberia
Maafisa wa afya wakiubeba mwili wa aliyekufa kwa Ebola LiberiaPicha: Dw/J. Kanubah

Huku hayo yakijiri,polisi nchini Guinea imewakamata watu 27 wanaoshukiwa kuwaua wahudumu wa afya na wanahabari waliokuwa katika ziara ya kuhamasisha jamii kuhusu Ebola.

Waathiriwa hao wanane walipotea baada ya ujumbe wao kuvamiwa na wakaazi waliokuwa na ghadhabu katika mji wa Womey wiki iliyopita. Waziri wa sheria wa Guinea Cheick Sacko hapo jana alisema jumla ya watu 27 wamekamatwa kuhusiana na kisa hicho na wanahojiwa na mwendesha mashitaka.

Baadhi ya raia wa Guinea wanaamini kuwa wahudumu wa afya wa kigeni wakishirikiana na wale wa Guinea walipanga njama ya kuanzisha ugonjwa huo kimakusudi au kuutumia kuwahadaa ili kuchukua damu na sehemu za viungo vyao vya mwili.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/Reuters/afp

Mhariri: Hamidou Oummilkheir