1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kupambana na Austria

20 Agosti 2011

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Löwe anatarajiwa wiki ijayo kutangaza kikosi kamili kitakachoshuka dimbani dhidi ya timu za Austria na Poland katika mechi za kufuzu kwa mashindano ya Euro 2012

https://p.dw.com/p/12KZJ
Chipukizi Mario GoetzePicha: dapd

Ujerumani inachuana na Austria mjini Gelsenkirchen tarehe 2 Septemba na dhidi ya Poland katika mechi ya kirafiki siku nne baadaye mjini Gdansk.

Frauen-Fußball-WM 2011 Viertelfinale Deutschland - Japan
Ndiyo uzalendoPicha: dapd

Kufuatia hayo, kocha huyo amemchagua kipa wa timu ya Hannover Ron Robert Zieler, kuwa katika kikosi hicho cha Ujerumani. Ni mara ya kwanza kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 kupata fursa kuichezea timu ya taifa.

Mkufunzi wa makipa Andreas Koepke ameuambia mtandao wa shirikisho la soka Ujerumani, DFB kuwa Zieler atakuwa kipa nambari tatu baada ya Manuel Neuer wa timu ya Bayern Munich, na Tim Wiese wa Werder Bremen.

FC St. Pauli - Hannover 96 0:1
Kipa Ron Robert ZielerPicha: picture alliance / dpa

Zieler ameipata nafasi hiyo kufuatia kuumia kipa wa Bayer Leverkusen, Rene Adler, na kwa mujibu wa Koepke, Zieler amefurahisha kwa umahiri wake tangu kulisimamia lango la Hannover, mwanzoni mwa mwaka huu, na ni sababu mojawapo kwa timu hiyo kupata nafasi katika mechi za kufuzu kwenye mashindano ya ligi ya Uropa.

Ama katika mechi za ligi ya Bundesliga, hapo jana Borussia Monchengladbach iliendeleza mwanzo wake mzuri katika msimu huu mpya kwa Marco Reus kuchangia mara mbili ushindi wa mabao 4-1, dhidi ya Wolfsburg, na kuizuia nafasi ya kwanza hapo jana jioni kwenye orodha ya ligi hiyo ya Bundesliga.

Fussball Bundesliga Saison 2011 2012 3. Spieltag Borussia Moenchengladbach - VfL Wolfsburg im Borussia Park
Marco Reus, kulia, na kipa Marc-AndrePicha: dapd

Baada ya kuifunga timu kuu Bayern Munich katika mechi ya ufunguzi Monchengladbach ilifufuka kutoka kufungwa bao moja kufuatia mkwaju wake Makoto Hasebe, uliopa Wolfsburg uongozi baada ya dakika 12.

Reus alilisawazisha hili dakika 3 baadaye, na penalti aliyoifunga Filip Daems ilifanya mambo kuwa mazuri na yakanawiri zaidi muda mfupi kabla ya kipindi cha mapumziko, kupitia bao la Raul Bobadilla. Reus aliongeza lake la pili kunako dakika 67 za mechi hiyo.

Monchengaldbach sasa ipo mbele ya Mainz ambayo haijafungwa mpaka sasa kwa pointi moja.

Kwengineko baadaye hii leo, FC Cologne iliyoanza kwa kupepesuka sana katika ligi hiyo ya Bundesliga, itajaribu kuwapozaa mashabiki wake mbele ya Kaiserslautern mjini Cologne.

Ligi hiyo ya Bundesliga itaendelea kesho kwa mechi mbili, ambapo Mainz wataikaribisha Schalke 04 huku Hanover 96 ikiwa mwenyeji wa Hertha Berlin.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Dpae/Afpe/Rtre
Mhariri: Yusuf Saumu