1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuirejeshea Namibia mabaki ya maiti

Yusra Buwayhid
29 Agosti 2018

Ujerumani Jumatano itarejesha mabaki ya maiti zilizochukuliwa kutoka Namibia karne moja iliopita, baada ya mauaji ya watu wengi wa makabila ya Herero na Nama, wakati wa ukoloni wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/33vEf
Mafuvu yaliyorejeshwa
Picha: Reuters/C. Mang

Ujumbe wa serikali ya Namibia utapokea mabaki hayo ambayo ni pamoja na mafuvu 19, ngozi ya kichwa na mifupa, wakati wa ibada maalumu ya kanisa huko mjini Berlin. Esther Utjiua Muinjangue, mwenyekiti wa Shirika la Mauaji ya Ovaherero, amesema ingekuwa ni fursa nzuri kwa Ujerumani kuomba msamaha kwa kile kinachotajwa mara nyingi kama mauaji ya kwanza ya kimbari ya karne ya 20.

Taifa linalojulikana sasa kama Namibia lilikuwa ni koloni la Ujerumani kuanzia mwaka 1884 hadi 1915, na wakati huo eneo hilo likijulikana kama Afrika ya Kusini-Magharibi.

Inasemekana kwamba baada ya kukasirishwa na vitendo vya walowezi wa Kijerumani vya kuwaiba wanawake wao, wanyama na ardhi ya jangwani, watu wa kabila la Herero walianzisha mashambulizi ya uasi Januari 1904.

Wapiganaji wake waliwaua raia wa Kijerumani 123 katika mashambulizi ya siku kadhaa. Kabila dogo la Nama nalo likajiunga na vuguvugu hilo mnamo mwaka 1905.

Malefu ya watu wa asili wa Namibia waliuawa, wakati walipokuwa wakipinga utawala wa kikoloni kati ya mwaka 1904 na 1908. Wengine waliuawa kutokana na njaa na mateso ya gerezani.

Wanahistoria wanakadiria kwamba watu 65,000 wa kabila la Herero na 10,000 wa kabila la Nama waliuawa. Idadi hiyo ilikuwa ni sawa na asilimia 80 na 50 ya idadi jumla ya watu wa makabila hayo.

Deutsch-Südwestafrika Zeichnung Hererokrieg Hereroaufstand
Vuguvugu la kabila la Herero katika Afrika ya Kusini-MagharibiPicha: picture-alliance/akg-images

Ujerumani haipo tayari kuomba radhi

Ujerumani haikuwahi kuomba radhi rasmi wala kutoa kutoa fidia yoyote ya moja kwa moja kwa mauaji hayo.

Watu wa makabila hayo ya Herero na Nama wamewasilisha kesi katika mahakama ya Marekani wakidai malipo kwa mauaji ya jamaa zao. Hakimu wa mahakama ya mjini New York bado hajatoa uamuzi iwapo ataisikiliza kesi hiyo ambayo Ujerumani inataka aaitupilie mbali.

Waziri mdogo katika wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Michelle Müntefering aliwaambia waandishi habari Jumatatu kuwa Ujerumani bado ina mengi ya kutafakari kuhusu suala la ukoloni. Mazungumzo yanayotarajiwa kuja na tamko la pamoja juu ya mauaji hayo bado yanaendelea kati ya nchi hizo mbili.

Leo itakuwa mara ya tatu mabaki ya maiti yanarejeshwa Namibia. Yaliletwa Ujerumani kwa mara ya kwanza kwa lengo la kufanyiwa utafiti ambao ulifanywa tena baadae dhidi ya Wayahudi wakati wa utawala wa Kinazi nchini Ujerumani.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp/dpa

Mhariri: Caro Robi