Ujerumani kuifanyia mageuzi sera ya misaada ya maendeleo | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.05.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Ujerumani kuifanyia mageuzi sera ya misaada ya maendeleo

Serikali ya Ujerumani inakusudua kufanya mageuzi katika sera yake ya misaada ya maendeleo kwa kupunguza idadi ya nchi zinazopokea misaada hiyo hadi nchi 60 tu.Vigezo vya haki za binadamu na utawala bora vitatumika.

Waziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller amesema orodha ya sasa ya nchi 85 zinazopokea misaada kutoka Ujerumani ni mzigo mkubwa unaoigharimu nchi hiyo dola bilioni 10.9 kila mwaka. Waziri huyo wa Ujerumani amezitaka nchi zinazopokea misaada kuielewa ishara hiyo na amefafanua juu ya vigezo vitakavyotumika katika kuamua kutoa misaada hiyo. Ameeleza kuwa nchi zitakazopokea misaada ni zile zinazozingatia utawala bora, zinazoheshimu haki za binadamu na zinazopambana na ufisadi. Waziri Müller amesema nchi zinazopinga mageuzi hazitaambulia kitu.

Wizara ya ushirikiano ya Ujerumani imefafanua dhana inayoitwa MBZ 2030 inayolenga shabaha zifuatazo: uhakika wa kupatikana chakula cha kutosha, afya na uzazi wa kupanga, elimu, nishati na ulinzi wa mazingira.

Kulingana na sera mpya inayokusudiwa, Ujerumani itatenga asilimia 25 ya bajeti ya misaada ya maendeleo kwa ajili ya kutekeleza elimu ya mafunzo ya kazi. Katika kutekeleza sera hiyo mpya,Ujerumani itaratibisha mipango yake kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya na pia na baadhi ya nchi, ikiwa pamoja na Ufaransa na Uingereza.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Ujerumani pia inakusudia kushirikiana na washirika wengine kama China, Urusi na Brazil kwa lengo hasa la kuendeleza juhudi ya kulinda uhai anuai, bahari na tabia nchi. 

Nchi ambazo Ujerumani imezitambua kuwa zinaendeleza mageuzi ni Tunisia, Ghana na Ethiopia. Na nchi zitakazowekwa kando ni Burundi kwa sababu ya kutozingatia utawala bora na Mynmar kwa sababu ya kukiuka haki za Warohingya.

Hata hivyo mwenyekiti wa mtandao wa Venro unaowakilisha mashirika ya misaada 140 ya nchini Ujerumani ameelezea wasi wasi juu ya sera hiyo mpya ya waizara ya ushirikiano ya Ujerumani. Mwenyekiti huyo Bernd Bornhorst amesema mdahalo wa kisiasa ni muhimu na ameeleza kuwa bila ya kupatiwa misaada nchi fulani zitadhoofika.

Chama cha upinzani cha waliberali, FDP pia kimeikosoa sera ya waziri Gerd Müller. Chama hicho kimesema sera ya bwana Müller itazipeleka nchi kadhaa kwenye mikono ya China. Shirika la misadaa la kanisa katoliki la Ujerumani limesema nchi zote maskini zinastahiki misaada na siyo zile tu zinazofanya mageuzi.

Wakati huohuo waziri Müller ametangaza mpango wa Euro bilioni moja kwa ajili ya kuziunga mkono nchi maskini zinazopambana na maambukizi ya virusi vya corona. Fedha hizo zitatumika katika juhudi za kuimarisha mifumo ya afya na uhakika wa kupatikana chakula. Nchi nyingi zinazoendelea hazina mifumo imara ya afya na huenda zikakumbwa vibaya sana na maambukizi ya virusi vya corona.

Chanzo:/DW