Ujerumani imeyakinisha urafiki na Israel | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.05.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani imeyakinisha urafiki na Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle Ijumaa (17.05.2013) ameyakinisha urafiki wa nchi yake kwa Israel katika kipindi hiki chenye changamoto kubwa katika eneo hilo kutokana na mzozo wa Syria.

Westerwelle na Netanjahu.

Westerwelle na Netanjahu.

"Nataka kusisitiza kwamba katika kipindi hiki cha changamoto ngumu Ujerumani inasimama pamoja na washirika wao wa Israell", Westerwelle amesema hayo wakati wa kuanza mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem ambaye alimwita mwenyeji wake huyo kuwa ni "rafiki mpenzi".

Ameongeza kusema kwamba wanataka kushirikiana nao,wanataka kuwaunga mkono kwani urafiki wao unamaanisha hivyo.Westerwelle amesema anatumia neno urafiki ambapo kwa uwelewa wao lina maana nzito zaidi kuliko washirika na kwamba ushirika wao sio tu wa mkakati bali ni urafiki kati ya jamii,kati ya wananchi na kati ya serikali.

Kwa upande wake Netanyahu amesema mageuzi makubwa ya ghafla yalioko hivi sasa Mashariki ya Kati ni makali zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa miongo mingi. Amesema leo Mashariki ya Kati inapitia kipindi cha ukosefu mkubwa wa utulivu ambacho hakina kifani.Waziri Mkuu huyo wa Israel ameongeza kusema kwamba hawakuwahi kushuhudia mageuzi makubwa kiasi hicho kwa miongo mingi katika eneo hilo.

Changamoto kubwa kwa Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle (kushoto) akilakiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. (17.05.2013)

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle (kushoto) akilakiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. (17.05.2013)

Netanyahu amesema anafuatilia kwa makini changamoto halisi kwa usalama wa Israel zinazosababishwa na mabadiliko hayo ya haraka. Netanyahu ameongeza kusema kwamba yuko tayari kwenda popote pale inapobidi na kukutana na yoyote yule inapohitajika na kwamba anachukuwa kile hatua inayohitajika kulinda usalama wa wananchi wa Israel ,jambo ambalo amesema ataendelea kulifanya.

Westerwelle pia amesema kwamba Ujerumani inaunga mkono kikamilifu juhudi za Marekani kufufuwa mazungumzo yaliokwama ya amani ya Mashariki ya Kati baina ya Israel na eneo zima la Mashariki ya Kati.Baada ya mkutano wake mjini Tel Aviv hapo Alhamisi na Waziri wa Sheria wa Israel Tzipi Livni, waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema wakati umefika wa kuanza kuzungumzia juu ya namna wanavyoweza kutowa mchango wao kwa kupitia hatua madhubuti ili fursa iliopatikana ambayo ndio kwanza imejichomoza iweze kutumika ipasavyo.

Livni ambaye ni afisa wa Israel anayeshughulikia mazungumzo na Wapalestina ameelezea imani yake juu ya fursa ya kufanikiwa kwa juhudi za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry.Livni amekaririwa akisema kwamba hamasa iliopo inaweza kuleta fursa mpya kwa amani Mashariki ya Kati.

Mashambulizi ya Israel kwa Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na Waziri wa Sheria wa Israel Tzipi Livni (17.05.2013 ) mjini Tel Aviv.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na Waziri wa Sheria wa Israel Tzipi Livni (17.05.2013 ) mjini Tel Aviv.

Westrerwelle hakutaka kuzungumzia moja kwa moja kuhusu mashambulizi ya anga ya Israel kwa Syria isipokuwa tu amesema kwamba Israel ina haki ya kujihami na kwamba yeye hana kitu cha kuongezea juu ya hilo.

Kwa mujibu wa repoti za vyombo vya habari Israel imeshambulia Syria kwa mabomu mara tatu tokea kuanza kwa mwaka huu kuzuwiya kusafirishwa kwa silaha za kisasa kwa kundi la wanamgambo wa Kishia la Hezbollah lilioko Lebanon.

Livni pia alishutumu makubaliano ya Urusi kuipelekea silaha Syria baada ya vyombo vya habari vya Marekani kuripoti kwamba shehena nyengine ya silaha imepelekwa kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad. Kauli yake hiyo pia inakuja kufuatia ziara ya ghafla ya mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani John Brennan kwa Israel kujadili hali ya Syria nchi jirani na Israel iliokumbwa na vita.

Ziara ya Westerwelle Mashariki ya Kati imegubikwa na suala la mchakato wa amani Mashariki ya Kati, vita vya Syria na mpango wa Iran unaoshukiwa kutengeneza silaha za nyuklia.Jumamosi (18.05.2013) Westerwelle amekutana na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Wapalestina anayeondoka madarakani Salam Fayyad huko Ukingo wa Magharibi kabla ya kuondoka kuelekea Algeria.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mwandishi : Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com