1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani ilifanya ujasusi dhidi ya Marekani

Mohammed Khelef
22 Juni 2017

Idara ya Ujasusi wa Kigeni ya Ujerumani (BND) ilikuwa ikiwachunguza maafisa kadhaa wa serikali na wafanyabiashara wa Marekani, wakiwemo wa Ikulu ya White House, linaripoti gazeti la kila wiki la Der Spiegel.

https://p.dw.com/p/2fAoa
Deutschland 60 Jahre BND
Picha: picture-alliance/dpa/H. Hanschke

Gazeti hilo limeandika kwenye toleo lake la leo (Alhamis, Juni 22) kwamba limeona nyaraka zinazothibitsha kwamba idara hiyo ya ujasusi ilikuwa na orodha ya majina 4,000 kwa ajili ya uchunguzi kati ya mwaka 1998 na 2006. 

Taarifa hizo zinajumuisha nambari za simu au faksi na pia anwani za barua pepe kwenye Ikulu ya Marekani na pia wizara za fedha na mambo ya nje za taifa hilo kubwa kabisa duniani.

Wengine waliolengwa kwenye uchunguzi walikuwa kwenye taasisi za kijeshi, kikiwemo kikosi cha anga na jeshi la ardhini, kituo cha uchunguzi wa angani (NASA) na hata shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch. 

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mamia ya balozi za kigeni na hata mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Fedha Duniani (IMF) hayakusalimika na uchunguzi huo.

Maafisa wa BND ilikataa kusema chochote kuhusiana na taarifa hiyo wakati gazeti la Der Spiegel lilipotaka maoni yao. 

Mwaka 2013, Ujerumani ilionesha kukasirishwa sana na taarifa zilizovujishwa na mkandarasi wa zamani wa Shirika la Usalama la Marekani (NSA), Edward Snowden, zilizoeleza kwamba maafisa wa kijasusi wa Marekani walikuwa wakinasa mawasiliano ya simu za watu kadhaa duniani, ikiwemo simu ya mkononi ya Kansela Angela Merkel.

Merkel, ambaye alikulia kwenye Ujerumani Mashariki chini ya mfumo wa kikomunisti ambako kuwachunguza raia  lilikuwa jambo la kawaida, alitangaza mara kadhaa kwamba "kuwafanyia ujasusi marafiki si jambo linalokubalika", ingawa huku akitambua utegemezi wa Ujerumani kwa Marekani kwenye masuala ya kiusalama.

Hata hivyo, kitu cha kilichokuja kuzua fadhaa kubwa kwa Ujerumani ni pale baadaye ilipokuja kudhihirika kuwa BND iliwasaidia NSA kuwachunguza washirika wa Ujerumani barani Ulaya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman