Ujerumani huenda isiondoe zuio la COVID-19 Januari 10 | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.12.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

COVID-19

Ujerumani huenda isiondoe zuio la COVID-19 Januari 10

Mkuu wa wafanyakazi wa serikali ya shirikisho ya Ujerumani, Helge Braun amesema hatua ya kuzifunga shughuli za umma nchini humo huenda zisiondolewe Januari 10. 

Helge amekiambia siku ya Jumataztu kituo cha televisheni cha RTL/ntv kwamba ana matumaini hatua kali zilizowekwa kuzuia kusambaa kwa visa vya virusi vya corona zitasaidia kupunguza maambukizi Ujerumani.

Amesema wakati huu wa msimu wa baridi, Ujerumani itashuhudia siku ngumu, ikizingatiwa kwamba bado chanjo ya virusi vya corona haijaanza kutumika humu nchini.

Kiongozi huyo wa wafanyakazi katika ofisi ya Kansela Angela Merkel amerudia kusema kuwa maduka, shule na vituo vya kuwaangalia watoto vitafungwa kuanzia Jumatano, ikiwa ni katika kuchukua hatua kali za kujaribu kudhibiti ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.

Uamuzi huo ulifikiwa jana katika mkutano wa Merkel na viongozi wa majimbo yote 16 ya shirikisho siku ya Jumapili ambapo walikubaliana kwamba hatua hizo kali zitadumu hadi Januari 10. Merkel amesema shughuli nyingi za kibiashara zisizo za lazima zitafungwa, ili kuzuia wimbi la pili la janga la virusi vya corona ambalo linautishia mfumo wa afya wa Ujerumani.

Deutschland Helge Braun

Mkuu wa wafanyakazi wa serikali ya shirikisho ya Ujerumani, Helge Braun

Merkel amesema Ujerumani inahitaji kuchukua haraka hatua ili kushughulikia ongezeko la maambukizi ya COVID-19, ingawa uamuzi huo unaweza kusababisha usumbufu mkubwa kwa wauzaji maduka, mfumo wa elimu na umma kuelekea katika msimu wa sikukuu ya Krismasi.

"Hatua inahitajika kuchukuliwa haraka kwa sababu hatua tulizoweka Novemba 2 hazikuwa za kutosha. Tulifanikiwa kupunguza ongezeko la maambukizi kwa muda na kupata utulivu, lakini kwa siku kadhaa tumeona ongezeko kubwa la idadi ya visa. Hii inamaanisha kwamba  tumeona vifo vingi, natumai mnafuatilia takwimu. Na tunajua kwamba mfumo wa afya tayari uko katika shinikizo kubwa," alifafanua Merkel.

Taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza ya Ujerumani, Robert Koch, siku ya Jumatatu imerekodi visa vipya 16,362 vya maambukizi ya corona, ambavyo ni visa 4,000 zaidi kuliko wiki moja iliyopita.

Nayo Italia, imeipiku Uingereza na kuwa taifa lenye idadi kubwa ya vifo vya COVID-19 barani Ulaya.

Ambrose Dlamini, Prime Minister Eswatini verstorben

Waziri Mkuu wa Eswatini, Ambrose Dlamini

Huku hayo yakijiri, Marekani Jumatatu inajiandaa kuanza mpango wa kutoa chanjo ya COVID-19 kwa wananchi wake, wakati ambapo vifo vitokanavyo na virusi hivyo vikielekea kufika 300,000.

Malori yenye vifaa muhimu kama vile majokofu yalitolewa nje ya kituo cha Kalamazoo, Michigan jana kama sehemu ya mpango wa umma na binafsi kupeleka mamilioni ya dozi za chanjo zilizoidhinishwa hivi karibuni za kampuni ya Pfizer na BionTech, kwa Wamarekani wenye uhitaji zaidi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Eswatini, Ambrose Dlamini amefariki dunia, wiki mbili baada ya kuugua virusi vya corona. Nchini Algeria, Rais Abdelmadjid Tebboune ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza, tangu alipolazwa baada ya kuugua COVID-19 mwezi Oktoba.

Huko Nigeria, takriban majenerali 26 wa jeshi wameambukizwa virusi vya corona baada ya kuhudhuria mkutano wa mwaka kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Abuja, wiki iliyopita. Kwa mujibu wa jeshi hilo, jenerali mmoja amefariki dunia.

(AFP, DPA, Reuters)