1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Hotuba ya mwaka ya Kansela Angela Merkel

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
19 Julai 2019

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amefanya mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin kabla ya kuanza mapumziko yake ya majira ya joto, ambapo amezungumzia masuala kadhaa kuhusu sera za ndani na nje ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/3ML9T
Angela Merkel Sommerpressekonferenz Berlin
Picha: Reuters/H. Hanschke

Katika mkutano huo na waandishi wa habari ambao hufanyika kila mwaka wakati wa majira ya joto, Kansela Merkel alimlaumu Rais wa Marekani Donald Trump kwa matamshi yake ya hivi karibuni dhidi ya wabunge wanne wanawake wa chama cha Democratic kutoka kwa jamii za walio wachache nchini Marekani akisema kuwa kauli hizo zinakwenda kinyume cha misingi ya Marekani.

Merkel amesema kwa mtazamo wake, nguvu za Marekani zinatokana na ukweli kwamba watu wa mataifa tofauti wamechangia kuiweka Marekani ilipo sasa.

Bibi Merkel alizungumzia pia kuhusu mvutano uliopo kati ya Marekani na Iran ambapo amesema kwa hakika unahitajika ufumbuzi wa kidiplomasia na kwamba anaunga mkono jitihada za Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron za kuanzisha njia za mawasiliano kati ya Iran na Marekani.

Kushoto: Annegret Kramp-Karrenbauer kiongozi wa CDU na waziri mpya wa ulinzi. Katikati Kansela Angela Merkel. Kulia: Ursula von der Leyen Rais mpya wa Halmashauri ya Ulaya.
Kushoto: Annegret Kramp-Karrenbauer kiongozi wa CDU na waziri mpya wa ulinzi. Katikati Kansela Angela Merkel. Kulia: Ursula von der Leyen Rais mpya wa Halmashauri ya Ulaya.Picha: Imago Images/IPON/S. Boness

Kuhusu Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya Kansela wa Ujerumani amesema ana furaha kwamba Umoja wa Ulaya hauna wasiwasi juu ya Brexit, na kwamba nchi wanachama wa umoja huo zitaendelea kulifanyia kazi suala hilo.

Bibi Merkel pia aligusia sheria ya ulinzi wa mazingira ya Umoja wa Ulaya, akimsifu mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg na wengi, wengineo ambao ni vijana kwa kuimarisha harakati za kuelimisha kuhusu umuhimu wa kutambua athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pia alitumia mkutano huo kuondoa mashaka juu ya afya yake, baada ya matukio matatu ya hivi karibuni ya kutetemeka yaliyosababisha wasiwasi nchini na nje ya nchi.

Merkel amesisitiza nia yake ya kuendelea na majukumu yake ya ukansela mpaka mwisho wa muhula wake. Kansela huyo wa Ujerumani, ambaye alitimiza miak 65 wiki hii, amesema hata yeye anajali sana maslahi ya afya yake binafsi.

Vyanzo:/DPA/Permalink https://p.dw.com/p/3MJL5