Ujenzi wa makaazi waisukuma Israel katika hali ya kutengwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ujenzi wa makaazi waisukuma Israel katika hali ya kutengwa

Israel huenda ikawapoteza marafiki zake

default

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Kutokana na sera yake ya ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika eneo la Jerusalem Mashariki, Israel imeendelea kukosolewa na jumuiya ya kimataifa. Marekani imekuwa ya kwanza kuitolea wito serikali ya Israel iachane na ujenzi wa makaazi hayo. Jana Umoja wa Ulaya, Ufaransa na Urusi nazo zikaurudia wito huo. Lakini serikali ya Israel imeipuuzilia mbali miito hiyo na kuimarisha udhibiti wa eneo la Jerusalem Mashariki. Mwandishi wetu Sebastian Engelbrecht katika maoni yake anasema Israel iko katika hatari ya kuupotoze urafiki na washirika wake muhimu.

Israel inawapoteza marafiki zake wazuri kabisa inayowategemea. Kwa mfano rais wa Marekani Barack Obama. Hatua ya Israel kukataa miito ya kuachana na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi ni pigo kubwa kwa rais Obama anayetaka kuunzisha tena mchakato wa kusaka amani ya Mashariki ya Kati. Rais Obama anataka ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Masahriki ukomeshwe. Lakini serikali ya Israel inayoongozwa na waziri mkuu Benjamin Netanyahu inaendelea kujenga nyumba zaidi katika maeneo ya Wapalestina, inateka ardhi ya Wapalestina na kuigawanya.

Ili kuiridhisha Marekani, waziri Netanyahu amesitisha ujenzi wa barabara kadhaa katika Ukingo wa Magharibi na kuruhusu kuvunjwa kwa makaazi kadhaa yanaolezwa kuwa yasiyo halali. Idadi ya makaazi ya walowezi wa kiyahudi inaendelea kuongezeka huku serikali ikifahamu na ikiridhia. Mnamo mwaka 1967 Israel ililichukua eneo la Jerusalem Mashariki na leo hii kuna walowezi takriban 500,000 wa kiyahudi wanaoishi katika eneo hilo. Waziri mkuu Netanyahu anataka kuifanya ardhi iliyo magharibi mwa mto Jordan, ambayo yeye mwenyewe aniita, Judea na Samaria, kuwa ya wayahudi na kuwafanya Wapalestina wanaoishi katika eneo hilo kuwa watu wa tabaka la pili. Na ijapkokuwa Netanyahu ameshazungumzia mpango wa kuundwa taifa huru la Palestina mwezi mmoja uliopita, lengo lake la dola kuu la kiyahudi la Israel, unabakia pale pale; mipaka inayoanzia bahari ya Mediterenia hadi Jordan.

Kwa mantiki hii, bwana Netanyahu ameiashiria Marekani kwamba ataendelea kupambana vikali kuhusu swala la ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika Jerusalem Mashariki. "Wayahudi wana haki ya kuishi mahala popote mjini Jerusalem na kujenga," ameshawahi kusema kiongozi huyo wa Israel. Hoja yake ni kwamba kama mtu angewapiga marufuku Wayahudi kuishi katika sehemu fulani za mjini London, New York, Paris au Roma, kungepigwa makelele na jumuiya ya kimataifa.

Netanyahu anaiona miito ya kuyavunja makaazi ya wayahudi katika Ukingo wa Magharibi kuwa na maana ya ubaguzi dhidi ya Wayahudi. Anayevuruga historia na wakati wa sasa hana haja ya kupigwa na mshangao wakati marafiki wazuri na anaowategemea watakapomuaga kwaheri.

Ikiwa waziri mkuu Netanyahu ataendelea kuongoza namna hii, Israel itawapoteza marafiki zake wazuri. Ikiwa kiongozi huyo wa chama cha Likud nchini Israel ataendelea hivyo, nchi yake pole pole itaingia katika hali ya kutengwa. Ishara tayari zimejitokeza kutokana na matamshi ya Ruprecht Polenz, mwenyekiti wa kamati ya mashauri ya kigeni katika bunge la Ujerumani. Mwanasiasa huyo wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, amesema Israel iko katika hatari ya kujitia kitanzi yenyewe kama taifa la kidemokrasia, iwapo itaendelea na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina. Polenz amenena kweli. Netanyahu anapoteza karata yake ya mwisho anaoicheza.

Mwandishi: Engelbrecht, Sebastian/ Charo, Josephat/ZR

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 22.07.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/IvPL
 • Tarehe 22.07.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/IvPL

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com