Uingereza yatakiwa kung′atuka haraka | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.06.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uingereza yatakiwa kung'atuka haraka

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameishinikiza Uingereza kuharakisha kujitowa Umoja wa Ulaya kwa kuonya kwamba haiwezi kumudu kuwa katika hali ya mkwamo na kwamba kujitowa huko hakuwezi kuwa kiurafiki.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi sita wanachama waasisi wa Umoja wa Ulaya waliokutana Berlin kwa mazungumzo ya dharura baada ya matokeo ya fadhaa ya kura ya maoni ya Uingereza wamesema serikali ya Uingereza inapaswa kuanza mchakato wa kujitowa haraka iwezekanavyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault amekwenda mbali zaidi kwa kumtaka Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ambaye amesema angelijiuzulu ifikapo mwezi wa Oktoba kumwachia nafasi haraka waziri mkuu mpya wa Uingereza aweze kusimamia kipindi cha mpito cha kujitowa kwenye umoja huo.

Wakati Umoja wa Ulaya ukikabiliana na uasi wake wa kwanza katika historia yake ya miongo sita Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean -Claude Juncker ameionya Uingereza dhidi ya kuburuza miguu hivi sasa wakati imekwishamuwa juu ya hatima yake.

Amekiri kwamba Umoja wa Ulaya ulikuwa ukitaraji Uingereza ingelibakia lakini sasa ni muhimu kuuharakisha mchakato wa kutengana bila ya kusababisha maumivu kwa kadri inayowezekana.

Uamuzi wa Cameron wakosolewa

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault akiwa na mawaziri wenzake.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault akiwa na mawaziri wenzake.

Rais wa bunge la Ulaya Martin Schulz ameuita uamuzi wa Cameron kusubiri kuondoka katika wadhifa wake hadi hapo mwezi wa Oktoba kuwa wa "aibu" amesema kwa kufanya hivyo "anaushikilia mateka umoja wote wa Ulaya".

Litakuwa jukumu la mtu atakayechukuwa nafasi ya Cameron kuongoza mazungumzo magumu chini ya Ibara ya 50 ya Mkataba wa Lisbon wa Umoja wa Ulaya ambao umeweka kipindi cha miaka miwili cha kujitowa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter- Steinmeir akiwa mwenyeji wa mawaziri wenzake watano wa mataifa yalioasisi Umoja wa Ulaya amesema wamekubaliana serikali ya Uingereza lazima ianze mara moja kutekeleza mchakato huo wa kujitowa.

Amewaambia waandishi wa habari "Tunaungana pamoja kusema kwamba mchakato huu lazima uanze haraka iwezekanavyo ili tusiishie kurefusha kipindi cha mkwamo na badala yake kulenga mustakbali wa Umoja wa Ulaya na kazi inayohitajika."

Uingereza ina wajibu kwa Ulaya

Akiambatana na mawaziri wenzake Ayrault wa Ufaransa, Bert Koenders wa Uholanzi, Paolo Gentiloni wa Italia, Didier Reynders wa Ubelgiji na Jean Asselborn wa Luxemburg, waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesisitiza kwamba Uingereza bado ina wajibu kwa Umoja wa Ulaya.

Koenders ametowa wito wa kuanza mara moja kwa mazungumzo ya nia njema na Uingereza kwamba "inabidi tusonge mbele.....inabidi tubadili ukurasa."

Waziri wa mambo ya nje Frank-Walter Steinmeier.

Waziri wa mambo ya nje Frank-Walter Steinmeier.

Steinmeier ameufunguwa mkutano huo kwa wito mzito kwa Umoja wa Ulaya iendelee kubakia kuwa kitu kimoja hata wakati wa dharura.Amesema ana imani kwamba nchi za umoja huo pia zitaweza kutuma ujumbe kwamba hazitomuachilia yoyote yule ainyukuwe Ulaya kutoka kwao.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye kwa kawaida ni mtu mwenye tahadhari amesema tu mazungumzo ya kujitowa kwa Uingereza "hayapaswi kujiburuza milele" na kwamba hadi hapo yatakapokuwa yamekamilishwa Uingereza itaendelea kubakia kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Ulaya ikiwa na "haki zote na wajibu".

Katika taarifa ya pamoja waliyoitowa baadae mawaziri hao wametetea njia refu na ya mafanikio ya Umoja wa Ulaya tokea inanze kwa shida hapo mwaka 1957.Lakini wamekiri kwamba umoja huo unahitaji kushughulikia ukweli kwamba sehemu ya jamii yao haina furaha kwa namna umoja huo unavyofanya kazi hivi sasa.

Mwandishi: Mohamed Dahman /AFP

Mhariri : Isaac Gamba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com