1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Uingereza kuwarudisha makwao wahalifu raia wakigeni

Tatu Karema
30 Januari 2023

Uingereza imechukua hatua mpya za kisheria kuharakisha mchakato wa kuwarudisha makwao wahalifu raia wakigeni na kuwabana baadhi ya wale waliodai hifadhi ya ulinzi chini ya sheria ya Uingereza

https://p.dw.com/p/4MtDu
Moldawien Airport Chisinau Jüdische Emmigranten auf Weg nach Israel
Picha: Tania Krämer/DW

Serikali ya Uingereza ilitaja kesi ya mbakaji mmoja aliyetiwa hatiani ambaye alikata rufaa kupinga uamuzi wa wizara ya mambo ya ndani wa kumfukuza kutoka Uingereza, kwa kudai kuwa ni mwathirika wa magenge ya uhalifu yanayojihusisha na biashara haramu ya binadamu. Wizara hiyo imeendelea kusema kuwa mbakaji huyo aliachiliwa kwa dhamana akisubiri rufaa, akafanya ubakaji mwingine na bado yuko nchini Uingereza.

Braverman asema sio haki kwa wahasiriwa wa kweli kusubiri muda mrefu

Katika taarifa, waziri wa mambo ya ndani Suella Braverman amesema sio haki kabisa kwamba wahasiriwa wa kweli wa utumwa wa kisasa wanaweza kuachwa wakisubiri kwa muda mrefu zaidi ili kupata ulinzi wanaohitaji kutokana na matumizi mabaya ya wazi ya kimfumo. Braverman ameongeza kuwa mabadiliko hayo yatakapoanza kutekelezwa, yatamaanisha kama umefanya makosa, wana uwezo wa kukataa ulinzi kwa mhalifu na kumfukuza Uingereza. Hatua zinazotekelezwa chini ya sheria mpya ya utaifa na mipaka inamaanisha kuwa wafanyikazi wa wizara ya mambo ya ndani, wanaweza kudai ushahidi wa utumwa wa kisasa, badala ya kusikiliza kauli za waathiriwa.

Mabadiliko yashtumiwa na makundi ya haki

Hii inaweza kujumuisha ushahidi kutoka kwa mfanyakazi wa msaada ama afisa wa polisi ambaye amesaidia kumuokoa mwathiriwa huyo. Lakini mabadiliko hayo yameshtumiwa na makundi ya kutetea haki kwa kuhujumu ulinzi kwa waathiriwa halali. Mpango mmoja wa Braverman wa kusafirisha wahamiaji hadi nchini Rwanda kwa ajili ya kupata makazi mapya ya kudumu, tayari umepingwa na mahakama.

Großbritannien | Suella Braverman
Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Suella BravermanPicha: Amanda Rose/Avalon/Photoshot/picture alliance

Mnamo mwezi Novemba, Shirika la Kitaifa la Uhalifu la Uingereza liliripoti kuwa makundi ya uhalifu hasa ya Waalbania, yalikuwa yanahujumu mfumo wa kuwatambua watu wanaokabiliwa na hatari ya utumwa wa kisasa ili kupata msaada unaostahili (NRM) unaofanyiwa marekebsiho chini ya sheria mpya. Mfumo huo wa ulibuniwa mwaka 2009. Ripoti hiyo ya shirika la uhalifu imesema kuwa, iwapo watapatikana wakifanya kazi katika mashamba ya bangi ama mashirika mengine ya uhalifu, wahamiaji wa Albania wamefunzwa kudai kuwa waathiriwa wa utumwa wa kisasa na kutuma maobi kwa NRM .

Mkataba mpya wa Uingereza na Albania

Mnamo mwezi Desemba, waziri mkuu Rishi Sunak, alitangaza mkataba mpya na Albania kuthibiti idadi ya wahamiaji kutoka nchi hiyo wanaovuka kutoka bara Ulaya.

Makubaliano hayo yalifanyika baada ya serikali ya Albania kutaka msamaha kwa kampeini ndhidi ya wahamiaji iliyopeperushwa katika vyombo vya habari nchini Uingereza kufuatia matamshi ya uchochezi kutoka kwa Braverman. Lakini waziri huyo amedumisha msimamo mkali na kufurahisha mrengo wa kulia wa kihafidhina unaotaka kuonesha kuwa Uingereza inaweza kuthibiti mipaka yake baada ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya na msako huo ni moja kati ya masuala ya kipaombele yalioahidiwa na Sunak kwa mwaka huu.

Katika taarifa siku ya Jumatatu (30.01.2023) Braverman amesema kuwa lazima wawakomeshe watu wanaohujumu sheria za uhamiaji na uhifadhi na kwamba amedhamiria kuwachukulia hatua wale wanaotumia vibaya ukarimu wa umma wa Uingereza .