1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yadai Iran ilijaribu kuizulia njia meli yake

Mohammed Khelef
11 Julai 2019

Uingereza inadai meli za kijeshi za Iran zilijaribu kuizuilia njia meli ya mafuta inayomilikiwa na Uingereza lakini zikaondoshwa na meli yake ya kivita, madai ambayo Iran inayakanusha vikali.

https://p.dw.com/p/3Lu8f
Kriegsschiff Royal Navy Type 23 Fregatte HMS Montrose
Picha: picture-alliance/AP/UK Ministry of Defence

Kwa mujibu wa Uingereza, mkasa huo ulitokea jana Jumatano kwenye mlango bahari wa Hormuz, muda mchache baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kurejelea vitisho vyake vya kuongeza vikwazo vikali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Awali, kituo cha televisheni cha Marekani, CNN, kiliripoti kuwa boti za Iran zilijaribu kuiteka meli hiyo ya mafuta ya Uingereza, lakini zikafurushwa na meli ya kijeshi ya Uingereza.

Hata hivyo, wizara ya ulinzi ya Uingereza ilisema kuwa mashua tatu za Iran zilijaribu tu kuizuilia njia meli hiyo iitwayo British Heritage inayomilikiwa na kampuni ya mafuta ya Uingereza, BP. 

"Kinyume na sheria za kimataifa, mashua tatu za Iran zilijaribu kuizuilia njia meli ya kibiashara, British Heritage, kwenye Mlango Bahari wa Hormuz. Meli ya kijeshi ya HMS Montrose ililazimika kujiweka baina ya mashua hizo za Iran na British Heritage na kutoa onyo la mdomo dhidi ya mashua ambazo kisha ziliondoka." Ilisema taarifa hiyo ambayo pia iliitolea wito Iran kujiepusha na kuichafua hali ya usalama kwenye eneo hilo.

Iran yakanusha

Hata hivyo, Kikosi cha Walinzii wa Mapinduzi ya Iran - chombo chenye nguvu kubwa za kijeshi ambacho Marekani inakilaumu kwa kufanya mashambulizi kadhaa dhidi ya meli za mafuta tangu mwezi Mei, kilikanusha vikali tuhuma za kujaribu kuiteka au kuizuilia njia meli hiyo ya mafuta ya Uingereza.

Iran Teheran - Hassan Rouhani hält Ansprache zum "Army Day"
Rais Hassan Rouhani wa Iran aliionya Uingereza kuwa ingelipatwa na matokeo mabaya.Picha: Getty Images/AFP

"Hakujatokea makabiliano yoyote ndani ya masaa 24 yaliyopita kati yetu na meli yoyote ya kigeni, zikiwemo za Uingereza." Ilisema taarifa fupi iliyotolewa na kikosi hicho.

Mkasa huu unachochea zaidi uhasama unaoendelea kwenye eneo hilo la Ghuba, ambalo tayari liko kwenye hatihati kutokana na mkwamo baina ya utawala wa Rais Trump wa Marekani na Iran juu ya mpango wa nyuklia wa taifa hilo la Kiislamu.

Siku ya Jumatano (11 Julai), Rais Hassan Rouhani aliionya Uingereza kwamba itakumbwa na matokeo mabaya ambayo hakuyataja, kufuatia hatua ya nchi hiyo kuikamata meli ya mafuta ya Iran kwenye eneo la Gibraltar.

Maafisa kwenye eneo hilo, ambalo linamilikiwa na Uingereza licha ya kuwa kwake Uhispania, walidai kuwa meli hiyo ilikuwa ikielekea Syria, ambayo imewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya, huku Marekani nayo ikiwa na vikwazo vyake dhidi ya mafuta ya Iran.

Iran ilikilaani kitendo hicho inachosema ni haramu, huku Uingereza ikikanusha madai ya maafisa ya Gibraltar kuwa imeishikilia meli hiyo kwa maagizo ya Marekani.