Uingereza kuongeza mbinyo dhidi ya Iran. | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Uingereza kuongeza mbinyo dhidi ya Iran.

Uingereza inaoneka kuongeza mbinyo wake dhidi ya Iran wakati waziri wa mambo ya kigeni Margaret Beckett anawafahamisha wabunge kuhusu mzozo unaozidi kukua , unaowahusu wanajeshi wanamaji 15 wanaoshikiliwa na Iran

.

Katika kile ambacho huenda ikawa ni awamu tofauti katika mzozo ambao waziri mkuu alizungumzia siku ya Jumanne, maafisa pia walitoa maelezo yanayohusu ushahidi wa uhakika kuwa wanajeshi hao walikuwa katika eneo la maji la Iraq wakati Iran ilipowakamata Ijumaa iliyopita, magazeti ya Uingereza yameripoti.

Uingereza inasisitiza kuwa wanamaji sita pamoja na wanajeshi wa kawaida saba ambao wanashikiliwa na Iran walikuwa wakifanya shughuli zao za kila siku za operesheni dhidi ya kuzuwia magendo wakati walipokamatwa katika eneo la maji la Shatt al-Arab kaskazini ya Ghuba siku ya Ijumaa.

Iran inasema kuwa wanajeshi hao waliingia katika eneo la maji la nchi hiyo, licha ya kuwa madai hayo yanapingwa na Iraq.

Beckett amekuwa katika ziara nchini Uturuki jana Jumanne, lakini alifupisha ziara yake hiyo ili kutoa maelezo katika bunge, baada ya kushindwa katika mazungumzo yake na waziri mwenzake wa Iran Manoucher Mottaki.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni amesema kuwa Beckett, alizungumza kwa ukakamavu sana na Mottaki.

Wakati huo huo Uingereza imetangaza leo kusisitisha uhusiano wote rasmi na Iran kuhusiana na suala hilo la kukamatwa kwa wanajeshi wake 15 nchini Iran. Akitoa tamko hilo waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Margaret Backett amesema kuwa ,

kama waziri mkuu alivyodokeza jana , tumo hivi sasa katika awamu mpya ya shughuli za kidiplomasia . Hii ndio sababu jeshi limetoa maelezo ya kina kuhusu tukio hilo, na ndio sababu nimeamua kuwa, tunahitaji kuelekeza juhudi zetu zote za kidiplomasia katika wakati huu ili kupata suluhisho la suala hili. Kwa hiyo tutasitisha kwa sasa mahusiano yote rasmi na Iran, hadi pale suala hili litakapotatuliwa.

Waziri Beckett alitoa maelezo hayo mara tu baada ya waziri mkuu Tony Blair muda mfupi kuahidi kuendeleza mbinyo dhidi ya Iran , ambapo amesema nchi hiyo inakabiliwa na kutengwa kabisa na jumuiya ya kimataifa. Waziri Beckett amesema hata hivyo kuwa sera nyingine kuihusu Iran zitaendelea kuangaliwa upya na kusonga mbele kwa tahadhari.

Taarifa hiyo imekuja baada ya maafisa wa kijeshi wa Uingereza walitoa maelezo ambayo wamesema yanaonyesha wanajeshi hao wakiwa umbali wa maili za baharini 1.7 ndani ya Iraq wakati walipokamatwa. Blair pia ameahidi kuongeza kasi ya mbinyo wa kimataifa dhidi ya Tehran , ambayo amesema inakabiliwa na kutengwa kabisa kimataifa kuhusiana na mvutano huo.

Nae waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Iran Manouchehr Mottaki akizungumza wakati wa mkutano wa jumuiya ya nchi za Kiarabu mjini Riadh, amesema kuwa Iran itamwachilia mwanajeshi pekee mwanamke miongoni mwa wanajeshi 15 wanaoshikiliwa na nchi yake.

Kukamatwa kwa wanajeshi hao wa Uingereza kumezusha mzozo mkubwa kati ya Uingereza na Iran , ambayo tayari inakabiliwa na mbinyo mkali kutoka mataifa ya magharibi kuhusiana na mpango wake wa kinuklia.

 • Tarehe 28.03.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHHJ
 • Tarehe 28.03.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHHJ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com