1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa Israel na Uturuki waharibika baada ya Gaza

Yusra Buwayhid
16 Mei 2018

Israel imetuma malori manane ya misaada ya kiutu pamoja na dawa za matibabu katika ukingo wa Gaza, huku uhusiano wake wa kidiplomasia na Uturuki ukiwa umeingia doa baada ya wanajeshi wa Israel kuwaua Wapalestina 60.

https://p.dw.com/p/2xnAH
Israel Protesten in Gaza | palästinensiche Frau dokumentiert die Lage
Picha: Getty Images/S. Platt

Israel imesema Jumatano kwamba imetuma malori manane yaliyojazwa misaada ya kiutu pamoja na dawa za matibabu katika ukingo wa Gaza, baada ya wanajeshi wake kuwaua Wapalestina wapatao 60 Jumatatu iliyopita kwa kuwafyatulia risasi katika eneo la mpaka kati ya Gaza na Israel. 

Kikosi cha kijeshi kwa masuala ya raia wa Palestina, Cogat, kimesema jana kwamba kimetuma tani 53 za vifaa vya matibabu huko Gaza, ikiwa ni pamoja na maji ya matibabu, bendeji na vifaa vya mazoezi ya mwili na kusema mafuta yatawasambazwa baadaye.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu jana alijitetea kwa kusema hakujakuwa na jinsi nyingine yoyote ya kukabiliana na waandamanaji hao zaidi ya kutumia nguvu ya kijeshi. Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Marekani cha CBS, Netanyahu alililaumu kundi la Kipalestina la Hamas.

"Natamani yasingetokea. Lakini Hamas inayashawishi makundi ya watu kujipenyeza Israel, na dhahiri wanatangaza lengo lao la kuitokomeza Israel," amesema benjamin Netanyahu.

Gazastreifen Proteste mit Steinschleuder
Wapalestina wakitumi manati huku wanajeshi wa Israel wakitumi risasi za moto katika maandamano ya GazaPicha: picture-alliance/NurPhoto/M. Faiz

Balozi zafukuzwa

Ujumbe wa kidiplomasia wa Palestina nchini Marekani umetakiwa kurudi nyumbani baada ya maandamano ya Jumatatu ya kupinga kufunguliwa ubalozi mpya wa Marekani mjini Jerusalem. Husam Zomlot amelithibitishia shirika la habari la AP kwamba ameitwa na serikali yake kurudi Palestina.

Wakati huo huo, Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan na Waziri Mkuu wa Israel wametupiana maneno na kuwataka wanadiplomasia wao kurudi nyumbani.

Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imemtaka balozi wa Israel kuondoka nchini mwake baada ya kukasirishwa na kitendo cha Israel cha kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji wa Kipalestina katika mpaka wa Gaza na uamuzi wa Marekani wa kuuhamishia ubalozi wake mjini Jerusalem. Kufuatia hatua hiyo, Israel nayo ikamtaka mkuu wa ubalozi mdogo wa Uturuki kuondoka kwa muda nchini mwake na kurudi Uturuki.Guatemala nayo Jamatatu imefuata mfano wa Marekani na kufungua ubalozi wake mjini Jerusalem.

Gaza Israel Konflikt Jerusalem US Botschaft
Binti wa Donald Trump, Ivanka Trump katika sherehe za kufungua ubalozi wa Marekani Jerisalem.Picha: Reuters/R. Zvulun

Juiya ya Kiarabu na Uturuki kuitisha mikutano

Vita vya maneno kupitia ukurasa wa Twitter kati ya Erdogan na Netanyahu vinatishia kuharibu makubaliano yao ya mwaka 2016 ya yaliyorejesha uhusiano wa kawaida baina yao baada ya mzozo wa miaka mingi.

Erdogan ataitisha mkutano wa kilele wa dharura Ijumaa ijayo mjini Istanbul wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Mataifa ya Kiislamu OIC, ambao amesema utatoa kauli nzito juu ya suala hilo la mauaji ya Wapalestina yaliyofanywa na Israel.

Mataifa ya Kiarabu kwa upande wake yamelaani mauaji hayo ya Wapalestina katika maandamno ya Jumatatu huko Gaza, kama ilivyo kawaida yao ya kufanya hivyo baada ya kila vurugu zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina. Lakini kutokana na hofu ya Iran walionayo baadhi yao, viongozi wa Kiarabau wamegawanyika juu ya suala hilo. Kuna ambao wako tayari kuiunga mkono Israel kisiri siri.

Jumuiya ya Kiarabu hata hivyo nayo pia itakuwa na mkutano hapo kesho Alhamisi ulioitishwa na Saudi Arabia kujadili mgogoro wa Israel na Palestina.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap/afp

Mhariri: Caro Robi