1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru wa vyombo vya habari Rwanda

Mwadzaya Thelma1 Mei 2007

Mei tarehe tatu ni siku ya kuadhimisha kumbukumbu ya kimataifa ya 17 ya uhuru wa vyombo vya habari.Suala muhimu linalojitokeza katika maadhimisho ya mwaka huu ni namna uhuru wa vyombo vya habari unavyobanwa na sheria za usalama huku ugaidi ukiendelea kuwa tishio katika jamii.

https://p.dw.com/p/CHF5
Kikao cha Mahakama za Gacaca
Kikao cha Mahakama za GacacaPicha: Deutsche Welle/Mark Caldwell

Waandishi nchini Rwanda wanachunguzwa na mashirika kadhaa ya kisheria katika shughuli za uandishi.Baraza la Vyombo vya Habari HPC nchini Rwanda ni moja ya mashirika hayo ikiwemo pia mahakama za Gacaca zilizoanzishwa baada ya mauaji ya halaiki ya mwaka 94.

Mahakama hizo hufuata mfumo wa kisheria unaotatanisha kwani kuna sababu za kisiasa zinazopelekea uamuzi wowote ule kutolewa.Mahakama hizo zinalaumiwa kutokuwa na msimamo wake maalum.Kwasababu ya utata huo serikali ya Rwanda imefadhaishwa na baadhi ya ripoti za kesi zilizotolewa na vyombo vya habari.Kwa upande wake serikali inakashifu vyombo vya habari na kuvilaumu kwa kuongeza chumvi.Hali yote hii inatatiza kujua ukweli ulipo.

Baadhi ya vyombo vya habari navyo vimeonyesha kuwa vinakubaliana na hoja hiyo ya kuwapaka waandisi wa habari tope.Hata hivyo serikali ya Rais Kagame sharti ikubali kuchukua lawama kuhusu namna inavyosuluhisha migogoro yao na waandishi wa habari.

Kwa sasa serikali inashughulikia matatizo hayo kwa kutumia njia za kisheria badala ya kujiondoa lawamani kutumia wizara yake ya mawasiliano.Hili linasababisha serikali kutaka usiri zaidi kwa mawaziri wake na kukataa kukosolewa na vyombo vya habari.

Tarehe 15 mwezi wa Januari watu wanne walivamia makazi ya Bonaventure Bizimuremyi ,mhariri wa gazeti la Umuco linalochapishwa kila baada ya majuma mawili.Watu hao waliharibu mali ya mwandishi huyo na kumtisha kuwacha kuandika makala zinazokashifu chama tawala cha Rwandan Patriotic Front RPF.

Gazeti la Umuco lilichapisha taarifa iliyohusu chama tawala cha RPF iliyoelezea uongozi mbaya kabla ya uvamizi huo kutokea.Hilo halikuwa tukio la kwanza.Mwaka 2005 mwezi Septemba maafisa wa usalama walizuia nakala ya gazeti hilo iliyomueleza Rais Kagame kama dikteta.Kulingana na maafisa hao taarifa hiyo huenda ingehatarisha usalama wa kitaifa.

Tangu wakati huo mwandishi mmoja wa gazeti hilo Jean Leonard Rugambage anazuiliwa korokoroni baada ya kuandika taarifa iliyoelezea vitendo vya rushwa serikalini.Mwezi Novemba tarehe 23 mwandishi huyo alishtakiwa kwa kudharau mahakama na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja.

Waziri wa Habari wa Rwanda alishtumu taarifa zilizoandikwa January 26 na waandishi wawili wa mashirika ya kimataifa Lucie Umukundwa wa Sauti ya Marekani VOA na Jean Claude Mwambutsa wa Shirka la Utangazaji la BBC.Kwa mujibu wa msemaji wa serikali Joseph Bideri aliye pia kiongozi wa kitengo cha mawasiliano na habari cha Rwanda ORINFOR,Jean Claude Mwambutsa aliongeza chumvi ripoti iliyotolewa na Shirika la Kutetea haki za binadamu nchini humo naye Bi Umukundwa alikashifu shughuli za baraza la vyombo vya habari.Shirika la waandishi wasio na mipaka Reporters Without Borders kwa upande wake lililaumu serikali kwa hatua hiyo ya kubana uhuru wa waandishi wa habari.

Mwaka 2006 mashirika yanayotetea uhuru wa vyombo vya habari yalitoa wito wa kuachiwa huru kwa waandishi watatu wa habari waliozuiliwa nchini Rwanda.Waandishi hao ni Rugambage,Tatiana Mukabibi na Dominique Makeli wa Radio Rwanda.Rugambage aliachiwa huru mwezi Agosti.

Ni katika mwezi huohuo ambapo mahakama kuu ya Rwanda ilithibitisha hukumu iliyosimamishwa kwa muda na faini ya takriban dola 1800 za marekani dhidi ya Charles Kabonero mhariri wa gazeti la Umuseso.Kabonero alipatikana na hatia ya kuandika matusi kwa umma kwasababu ya taarifa aliyoandika iliyokashifu serikali.Mwezi Aprili mhariri huyo alipakwa matope na baadhi ya magazeti yaliyodai kwamba alihusika kwa karibu na jeshi katika njama ya kujaribu kupindua serikali.Madai hayo yalichunguzwa na shirika la kutetea haki za waandishi la RSF na kupatikana kuwa si kweli.