1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Vyombo vya habari

Uhuru wa kujieleza redioni waminywa Tanzania

13 Februari 2018

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Redio, wadau wa redio Tanzania wanasema waandishi wa habari wa radio wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kutokana na kupokonywa kwa haki ya kujieleza.

https://p.dw.com/p/2saB1
Mkulima akisikiliza redio
Picha: B. Salouka

Kila mwaka, tarehe 13 Februari, dunia inaadhimisha Siku ya Redio. Ni wasaa wa kukumbuka kwamba bila ya matangazo ya redio, mamilioni ya watu wasingeliweza kupata habari licha ya kukua kwa teknolojia hasa katika maeneo ambayo mitandao ya intaneti haifiki kwa urahisi. Wadau wa sekta ya redio Tanzania wanataja miongoni mwa mengine sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari, pamoja na hofu ya wamiliki kufungiwa matangazo, kuwa vinachangia kurudisha nyuma maudhui ya redio hivyo kusalia katika vipindi vya kuburudisha pekee.

Maadhimisho haya yana maana nyengine kwa baadhi ya wadau wa mausuala ya redio Tanzania, ambao wanahoji kuwa bado waandishi wa habari wanaminywa na sheria zilizo na maslahi kwa mamlaka pekee. Hali hii, wanasema, inavifanya vituo vingi vya redio kujikita katika habari za kuwapendelea wanasiasa na kusahau wajibu hasa wa redio.

Waandishi wako chini ya uangalizi mkali

Kajubi Mukajanga, mkurugenzi mtendaji wa Baraza la Habari la Tanzania, ameiambia DW kuwa licha ya kuwepo kwa vituo vingi vya redio nchini, bado maudhui hayaridhishi kutokana na kuminywa kwa uhuru wa habari.

Lakini si la uhuru pekee linalouminya uhai na dhima ya redio. Kuna pia suala la utandawazi, ambalo nalo linatazamwa katika kuzifanya redio hapa nchini kuwa katika mifumo ya kisasa kufuatana na kukuwa kwa teknolojia duniani. 

Licha ya redio imekuwa ikitegemewa kwa kiwango kikubwa kwa watu walio katika maeneo ya vijijini kupata taarifa, waandishi wanasema bado wamekuwa katika ukakasi mkubwa wa kuandika taarifa kutokana na wengi kuwa chini ya uangalizi mkali. Hofu yao ni kuwa jumuiya ya kimataifa itaanza kuitazama Tanzania kama si sehemu salama kwa uhuru wa habari.

Kauli mbiu ya Siku ya Redio mwaka huu ni Redio na Michezo, huku msisitizo mkubwa ukitolewa kwenye suala zima la utandawazi katika michezo pamoja na suala la usawa wa kijinsia.

Mwandishi: Hawa Bihoga

Mhariri: Mohammed Khelef