Uhuru kwa Kosovo ? | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 04.04.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Uhuru kwa Kosovo ?

Baraza la Usalama la UM lilishauriana jana huko New York mpango wa mjumbe wake Ahtisaari juu ya hatima ya mkoa wa serbia-Kosovo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilizingatia jana hatima ya jimbo la Kosovo.Mjumbe maalumu wa UM kwa mkoa huo Martti Ahtisaari,aliutangaza rasmi mpango wake juu ya mustakbala wa Kosovo:

Amependekeza Kosovo iwe dola huru chini ya usimamizi wa jumuiya ya kimataifa.Wakati Marekani na washirika wake waungamkono pendekezo hilo ,Urusi inatetea kuwa jimbo la Kosovo linalokaliwa na waalbania wengi mno, lisalie chini ya mamlaka ya Serbia.

Baada ya kikao cha faragha cha masaa kadhaa hapo jana, hakujaibuka dalili ya maafikiano ya haraka juu ya kupewa uhuru jimbo la Kosovo.

Kwa muujibu wa mjumbe wa Marekani Wolff,kunahitajika wakati zaidi kwa mashauriano ili kuuzingatia barabara mpango wa Bw.Ahtisaari.Bw.Ahtisaari binafsi alieleza siku ya jana kuwa –siku muhimu ya kuendeleza mbele utaratibu ambao unahitaji pumzi ndefu.Alisema:

Nisingependa kuziita mbio za marathon ,lakini yamkini zikawa za mita 10.000.”

Na vikwazo gani viko njiani mwa mbio hizo za masafa marefu ilibainika wazi siku ya kwanza hapo jana ya mashauriano katika Barazya la Usalama la UM.Kwani, rais wa Serbia , Vojislav Kostunica kwa mara nyengine tena alipinga pendekezo hilo la Bw.Ahtisaari na akashauri mpango wake utupiliwe mbali na ateuliwe mjumbe mpya.

Matamshi hayo yalikataliwa haraka na mjumbe wa Uingereza katika Umoja wa mataifa John Perry:

“Dhana zote kuwa mapendekezo hayo hatuyakubali au litafutwe suluhisho jipya ni kupotosha mambo.”

Hatahivyo, Bw.Perry aliungama kuwa, katika Baraza la Usalama kuna sauti nyingi zinazoungamkono pendekezo la Russia la kupeleka Kosovo Tume ya kuchunguza ukweli kutoka Baraza la Usalama .

Ufaransa hapo ikaonya pasifanywe jaribio la kuuzorotesha utaratibu wa kuleta ufumbuzi wa mgogoro wa Kosovo.Hata Fatmir Sejdiu, rais wa Kosovo ambae mwanzoni mwa mashauriano haya alifunga safari ya New York, aliweka wazi kuwa wananchi wake wanasubiri kwa hamu kuu uamuzi na wana haki ya kujua mustakbala wao.

“Umma wa Kosovo, unasubiri na nadhani una haki ya kujua mustakbala wake.”

Lakini, kwa sura ya hali ya mambo inavyoonekana, patahitajika subira zaidi hadi pale litakapopitishwa azimio na Baraza la Usalama la UM .Bila ya azimio hilo, mpango wa Bw.Ahtisaari hautaweza kutekelezwa .

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com