Uhispania na Morocco zazozana kuhusu wahamiaji | NRS-Import | DW | 18.05.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Uhispania na Morocco zazozana kuhusu wahamiaji

Uhispania imetuma wanajeshi katika kisiwa cha Ceuta, kupiga doria katika mpaka wake na Morocco baada ya maelfu ya wahamiaji kuogelea na kuingia katika eneo hilo la Kaskazini mwa Afrika.

Wanajeshi wakiwa ndani ya magari ya kivita wanalinda pwani ya Cueta huku wahamiaji kadhaa waliokuwa wakiogelea na kukaribia ufukweni wakionekana kusogea mbali na mahali wanajeshi waliposimama. Mamia ya wahamiaji wengine walisimama upande wa uzio wa Morocco ambao hutenganisha kisiwa hicho cha Uhispania na Morocco.

Video zinazosambazwa mitandaoni zinaonesha wahamiaji wakiingia Ceuta kwa kuogelea na kupanda juu ya uzio bila ya kuzuiliwa na mamlaka za Morocco.

Kulingana na baadhi ya wataalamu, Morocco hutumia mbinu ya kuwaruhusu wahamiaji kuingia katika kisiwa cha  Ceuta ili kuiwekea shinikizo Uhispania, ambayo iliikasirisha Morocco mwezi uliopita kwa kukubali kiongozi wa waasi wa chama cha Polisario cha Sahara Magharibi kulazwa katika hospitali moja nchini Uhispania.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uhispania Fernando Grande-Marlaska amesema takriban wahamiaji elfu sita, miongoni mwao watoto wapatao 1,500, waliogelea na kuingia Ceuta siku ya Jumatatu na Jumanne na kuongeza kuwa karibu 2,700 walikuwa tayari wamerudishwa Morocco.

Angola | Besuch Pedro Sanchez in Luanda

Pedro Sanchez, waziri mkuu wa Uhispania

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez ameapa kurejesha utengamano na sheria katika kisiwa cha Ceuta na katika mipaka ya Uhispania haraka iwezekanavyo, akiongeza kuwa atakitembelea kisiwa hicho pamoja na kisiwa cha Melila baadaye leo.

Morocco yahimizwa kuwazuia wahamiaji haramu

Wakati haya yakiarifiwa, Umoja wa Ulaya umeihimiza Morocco kuzuia uingiaji wa wahamiaji kinyume cha sheria katika kisiwa cha Ceuta.

Wahamiaji hao walianza kumiminika Ceuta Jumatatu, wengi wao wakiogelea na kuvuka kwa miguu katika pwani ya kisiwa hicho ambacho ni himaya ya Uhispania, wakati bahari ilipokuwa imekupwa. Idadi ndogo ya wahamiaji 86 wamefanikiwa kuingia Melila ambacho ni kisiwa kingine cha Uhispania nchini Morocco.

Kamishna  wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia masuala ya ndani Ylva Johansson ameliambia bunge la Ulaya kwamba kuwasili kwa wahamiaji huko Ceuta ni tukio ambalo halikutarajiwa na linalotia wasiwasi na kudokeza kuwa idadi kubwa kati yao ni watoto.

"Kitu cha muhimu zaidi ni vipi Morocco itakavyoendelea kujitolea kuwazuia wahamiaji kuondoka nchini kwa njia isiyo halali na kwamba wale wasio na haki ya kukaa wanarejeshwa kwa njia muafaka. Mipaka ya Uhispania ni mipaka ya Ulaya. Umoja wa Ulaya unataka kujenga uhusiano na Morocco uliojikita katika msingi wa kuaminiana na kujitolea kwa dhati, na uhamiaji ni kipengee muhimu katika kuifikia azma hii."

Johansen amesema yeye pamoja na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borell wanawasiliana na maafisa wa Uhispania kuhusu suala la wahamiaji linaloshuhudiwa sasa.

Akionyesha mshikamano na serikali ya mjini Madrid, Rais wa baraza la Ulaya Charles Michel amesema katika ujumbe wake aliouandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba mipaka ya Uhispania ni mipaka ya Umoja wa Uaya. Michel alliongeza kuwa ushirikiano, uaminifu na kujitolea kwa dhati kwa pande zote mbili ni mambo yanayotakiwa kuwa kanuni muhimu za msingi wa mahusiano imara kati ya Umoja wa Ulaya na Morocco.

(reuters,afpe)