1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhalifu wa mipakani wawakutanisha wanasheria

6 Juni 2017

Wanasheria na waendesha mashitaka wa Afrika Mashariki wanakutana Arusha kaskazini mwa Tanzania kusaka mbinu mpya za kukabiliana na uhalifu unaovuuka mipaka katika wakati ambapo mataifa ya kanda hiyo yakipigania umoja.

https://p.dw.com/p/2eC5t
Symbolbild Mord Ehrenmord Messer
Picha: bilderbox

Mkutano huo unawashirikisha wataalamu wabobezi wa sheria za kimataifa na watetezi wa haki za binadamu, wasomi na wanaharakati, ambao kwa pamoja watashiriki katika kujadili mbinu na miapango ya kisheria katika kukabiliana na uhalifu dhidi ya ubinadamu na uwajibikaji wa wahusika wa matukio hayo mbele ya sheria.

Huu ni mkutano wa ngazi za juu katika masuala ya sheria na uendeshaji wa mashitaka katika nchi za Afrika Mashariki, katika wakati ambapo waendesha mashitaka wanaelezea kukabiliwa na changamoto za kukosekana kwa majaji wenye uwezo wa kuendesha kesi pamoja na ulinzi dhidi ya mashahidi wa kesi hizo, hali inayosababisha kuchelewa kwa hukumu dhidi ya kesi hizo.

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Uganda, William Byaruhanga, anasema kuwa pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo katika kesi za uhalifu wa kutoka nje, bado wameweza "kushuhudia mafanikio kadhaa katika kesi mbalimbali ikiwemo kesi ugaidi iliyomalizika hivi karibuni."

"Ushirikiano katika nyanja za upelelezi na kubadilishana wahalifu ndio iliyotuwezesha kupata ushahidi na hata wahusika wa tukio hilo", anasema Byaruhanga akiongeza kuwa ushirikiano baina yao utawezesha kukomesha uhalifu wa kutoka nchi moja hadi nyingine.

Akizungumzia kesi za aina hiyo, Mkurugenzi wa Mashitaka wa Tanzania Bara, Biswalo Mganga, amesema nchi yake imeweza kuweka rikodi ya mafanikio katika kesi mbalimbali "zikiwemo za uhalifu wa kimtandao na fedha haramu katika siku za hivi karibuni."

Mkutano huo pia utashuhudia kuzinduliwa kwa mradi wa kupambana na uhalifu na ufisadi uliosasisiwa na asasi ya kimataifa ya WAYAMO na kufadhiliwa na serikali ya Ujerumani.

Mradi huo pia una lengo la kuangazia uwezeshaji wa ofisi za waendesha mashitaka kwa kuzijengea uwezo na kuhakikisha kuwa utawala wa sheria na haki za binaadamu unazingatiwa kama njia muhimu ya kukabiliana na uhalifu.

Mwandishi: Charles Ngereza/DW Arusha
Mhariri: Mohammed Khelef