Ugiriki yafikia makubaliano ya muda na wakopeshaji | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ugiriki yafikia makubaliano ya muda na wakopeshaji

Serikali ya Ugiriki imepata muda zaidi wa kuweza kulipa madeni yake baada ya kufikia makubaliano na wakopeshaji wake katika mazungumzo mapana yaliyofanyika hapo jana

Shirika la fedha la Kimataifa – IMF limesema serikali ya Ugiriki ililiomba kuikubalia kulipa katika fungu moja mnamo Juni 30, madeni yake yaliyotarajiwa kulipwa mwezi huu wa Juni.

Ugiriki ambayo inakabiliwa na matatizo ya kifedha, ilistahili kulipa leo Ijumaa deni la kiasi cha euro milioni 300 kwa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF na malipo mengine baadaye mwezi huu ya jumla ya karibu euro bilioni 1.6. Lakini sasa imeruhusiwa na IMF kuyaweka pamoja mafungu manne yaliyotarajiwa kulipwa leo na badala yake kulipa fungu moja la euro bilioni 1.6 mnamo Juni 3.

waziri wa Uchumi wa Ugiriki George Stathakis amesema Ugiriki haiwezi kuyakubali mapendekezo ya karibuni yaliyowekwa kwenye meza ya mazungumzo na wakopeshaji wake wa kimataifa wa mpango unayoitaka ifanye mageuzi muhimu kabla ya kupewa fedha za mkopo. Waziri huyo hata hivyo amesema wako tayari kujadiliana ili kufikia maelewano.

Yanis Varoufakis

Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis

Alipoulizwa ikiwa Ugiriki imejiandaa kuondoka katika kanda ya sarafu ya euro, Stathakis alisema chama chake cha Syriza, kilichochaguliwa mwezi Januari baada ya kuahidi kumaliza mpango wa kubana matumizi, hakijapewa jukumu la kufanya hivyo na watu wa Ugiriki.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Usalama wa Jamii Dimitris Stratoulis ambaye ana msimamo mkali serikalini alisema serikali ya Ugiriki inayoongozwa na chama cha siasa za mrengo wa kushoto huenda ikaamua kuitisha uchaguzi wa mapema ikiwa wakopeshaji wake wa kimataifa hawatalegeza masharti yao.

Stratoulis anaegemea chama tawala cha mrengo wa siasa kali za kushoto Syriza, na haijafahamika ikiwa kauli yake inaiuwakilisha mtazamo mpana ndani ya chama hicho. Lakini imedhihirisha hasira kubwa kutokana na mapendekezo ya wakopeshaji wa kimataifa na kuongezeka hisia kuwa chama hichi kitatafuta njia mbadala za kuepuka kuukubali mpango huo.

Na wakati mgogoro huo wa kifedha ukiendelea, uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa karibu robo tatu ya Wagiriki wanaunga mkono kubakia katika kanda ya sarafu ya euro, wakati idadi kubwa ya Wagiriki wakiunga mkono kuwepo makubaliano katika mazungumzo yanayoendelea na wakopeshaji wa ili kuondoa mkwano uliopo.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na tovuti ya habari ya Newsit, asilimia 74 ya Wagiriki inaunga mkono sarafu ya euro, wakati asilimia 18 ikipendelea kurejea katika sarafu ya taifa la Ugiriki. Pia ulipata kua asilimia 50 ya watu wanaunga mkono kuwepo maelewano mapana wakati nao asilimia 40 wakipinga.

Waziri mkuu Alexis Tsipras anatarajiwa kukihutubia kikao cha dharura cha bunge baadaye leo wakati mgawanyiko ukiendelea kushuhudiwa ndani ya chama chake cha Syriza.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com