1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki: Tutapata usaidizi kutoka nchi nyengine

Mjahida10 Februari 2015

Waziri wa ulinzi wa Ugiriki Panos Kammenos amesema iwapo nchi hiyo itashindwa kupata makubaliano na kanda ya nchi zinazotumia sarafu ya Yuro kuhusu deni lake, inaweza kutafuta usaidizi kutoka mataifa mengine.

https://p.dw.com/p/1EYyv
Waziri wa ulinzi wa Ugiriki Panos Kammenos na Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras
Waziri wa ulinzi wa Ugiriki Panos Kammenos na Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: AFP/Getty Images/L. Pitarakis

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Ugiriki, Waziri Panos Kammenos amesema na hapa ninamnukuu "Kile tunachotaka ni makubaliano lakini iwapo makubaliano hayo hayatafikiwa na tukiona Ujerumani ina ugumu kutekeleza hayo na inataka kuisambaratisha Ulaya basi tutakwenda katika mpango wa pili ambao ni kupata fedha kupitia chanzo kingine." Mwisho wa kumnukuu.

Waziri huyo amesema huenda Marekani, Urusi, China au mataifa mengine yakawa katika orodha ya mataifa yatakayoombwa msaada.

Kammenos ni kiongozi wa chama cha kizalendo cha Independent Greeks kinachopinga mpango wa kubana matumizi ambacho ni chama kidogo kilichoungana na chama cha mrengo wa kushoto cha Syriza cha Waziri Mkuu Alexis Tsipras.

Ugiriki inatafuta makubaliano mapya na kanda inayotumia sarafu ya Yuro ili kujiondoa katika mpango wa kubana matumizi uliowekwa kama sharti la nchi hiyo kupata mkopo wa kujikwamua na madeni na nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na shirika la fedha la Kimataifa IMF mwaka 2010.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: REUTERS/ Alkis Konstantinidis

Ujerumani haina nia ya kulegeza masharti kwa Ugiriki.

Hata hivyo nchi za kanda ya yuro na hasa Ujerumani haijaonesha nia yoyote ya kulegeza masharti yake kwa Ugiriki. Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble, amesema iwapo Ugiriki inataka usaidizi inapaswa kuwepo na mpango utakaokubaliwa na wakopeshaji badala ya kufikiria usaidizi wa dharura.

Aidha Waziri Mkuu Alexis Tsipras atakutana siku ya Jumatano na na Angel Gurria, mwenyekiti wa shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo kuzungumzia pendekezo la Ugiriki ya kutokuwa na masharti ya kubana matumizi siku moja kabla ya kufanyika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels siku ya Alhamisi.

Hata hivyo kabla ya mkutano huo muhimu,rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker ameitahadharisha Ugiriki juu ya kujitenga na Umoja huo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/M. Rehle

Halikadhalika Juncker ameitaka Ugiriki kutofikiria kwamba mtazamo wa Umoja huo umebadilika na kwamba nchi zinazotumia sarafu ya Euro zinaweza tu kuridhia mapendekezo ya Waziri Mkuu Tsipras bila ya masharti.

Akizungumza siku moja baada ya mkutano wa Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya, Juncker ameongeza kuwa hataraji makubaliano yoyote kufikiwa juu ya Ugiriki katika mkutano jumla wa Umoja huo mjini Brussels.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu