Ugiriki na Japan zatoka sare tasa | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 20.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Ugiriki na Japan zatoka sare tasa

Ugiriki iliyocheza wachezaji kumi iliiteka Japan kwa kutoka sare ya kutofungana goli ambayo haitazifaidi timu zote mbili katika mchuano huo wa kundi C, ambao uliipa kibali Colombia kuingia 16 za mwisho

Timu zote mbili zilikuwa zikitafuta ushindi ili kurejesha matumaini yao ya kuendelea mbele baada ya kushindwa katika mechi zao za ufunguzi, lakini Ugiriki ndiyo itakayokuwa na furaha zaidi baada ya kucheza kwa dakika 52 bila ya nahodha wake Kostas Katsouranis, ambaye alitimuliwa uwanjani kwa kufanya makosa yaliyompa kadi mbili za njano.

Japan iliutawala mchezo lakini haikuweza kuzitumia vyema nafasi zake chungu nzima ilizotengeneza katika safu ya ulinzi ya Ugiriki ambayo kwa mara nyingine tena ilionekana kama ni ile ambayo ilifungwa magoli manne katika mechi kumi za kufuzu katika Kombe la Dunia nchini Brazil.

Japan, mabingwa wa bara Asia ambao walianza kampeni yao kwa kichapo cha magoli mawili mikononi mwa Cote d'Ivoire, waliendeleza mfumo wao wa mashambulizi ambao uliifanya kuwa timu ya kwanza kufuzu katika tamasha la Brazil lakini watastahili kuwabwaga Colombia katika mchuano wao wa mwisho ili wawe na nafasi ya kuendelea mbele.

Colombia waongoza kundi C na points 6 kutokana na mechi zake mbili, mbele ya Cote d'Ivoire ambao wana points 3. Japan wanashuka dimbani na Colombia Jumanne mjini Cuiaba wakati Ugiriki wakikutana na timu hiyo ya Afrika mjini Fortaleza.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com