Uganda yathibitisha kifo cha ebola | Matukio ya Afrika | DW | 12.06.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Uganda yathibitisha kifo cha ebola

Uganda imethibitisha kifo cha kwanza kilichotokana na ugonjwa wa ebola.

Kijana wa umri wa miaka 5 aliyekuwa akitapika damu amekuwa mtu wa kwanza kufariki kutokana na ugonjwa hatari wa ebola nchini Uganda. Hiki ni kisa cha kwanza cha ebola nje ya taifa jirani la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako maafisa wanajaribu kuchunguza jinsi familia ya kijana huyo, ambayo ilikuwa katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo, ilivyofanikiwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Uganda.

Shirika la afya duniani WHO lilithibitisha Jumanne jioni kisa cha kwanza cha ebola nje ya Congo tangu ugonjwa huo ulipolipuka mwezi Agosti mwaka uliopita. Karibu watu 1,400 wamekufa kutokana na ugonjuwa huo.

Wizara ya afya ya Congo inasema jamaa kadhaa wa familia ya kijana huyo walikuwa wameonyesha dalili za ebola na walikuwa wamewekwa karantini. Lakini sita walifanikiwa kuondoka wakati wakisubiri kuhamishiwa katika kituo maalumu cha matibabu ya ebola. Maafisa wanasema watu hao waliingia Uganda, ambako kijana huyo alikuwa akitibiwa na jamaa zake wakitengwa wasitangamane na watu wengine.

Wataalamu wamekuwa wakihofia kwa muda mrefu kwamba ugonjwa wa ebola huenda uungesambaa katika mataifa jirani kwa sababu ya machafuko yanayokwamisha kazi ya utoaji wa huduma za afya zinazonuiwa kuudhibiti ugonjwa huo nchini Congo.

(ape)