1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUganda

Uganda yashuhudia vifo zaidi ya 100 vya ajali za barabarani.

6 Januari 2023

Watu 16 wamefariki katika ajali ya barabarani iliyotokea usiku wa kuamkia leo na kufanya watu waliokufa kwa ajali hizo katia muda wa wiki mbili kuwa zaidi ya 100.

https://p.dw.com/p/4LoVB
Straßen von Kampala, der Hauptstadt von Uganda
Picha: picture-alliance/AA/A. Lubowa

Raia wa Uganda wamepokea habari za vifo vya watu 16 kwa ajali nyingine ya barabarani iliyotokea usiku wa kuamkia leo kwa hisia mseto za huzuni, hofu na hasira.  Ajali hii imepelekea idadi ya waliofariki katika ajali za barabarani katika muda wa wiki mbili tu nchini humo kuwa zaidi ya watu 100. 

Kulingana na takwimu za polisi wa usalama barabarani tangu tarehe 23 mwezi Desemba mwaka jana, angalau watu 55 walifariki katika muda wa siku tatu kati ya tarehe 23 na 26 mwezi Desemba wakati watu walipokuwa katika pirikapirika za kwenda kwenye likizo ya Krismasi.

Tangu tarehe 26 hadi jana watu walioripotiwa kupoteza maisha yao kutokana na ajali za barabarani ilikuwa imefikia watu 86 na hii leo idadi hiyo imezidi kwa watu 16 kufuatia ajali ya mkesha wa leo kaskazini mwa Uganda. Msemaji wa polisi wa usalama barabarani, Faridah Nampiima, amethibitisha kisa hicho.

DW-Sendung | Corona und die Menschenrechte | High-Res-Still
Visa vya ajali za barabarani vimeibua malalamiko kutoka kwa jamii dhidi ya mamlaka zinazosimamia eneo hilo.Picha: DW

Taarifa za awali zinaelezea kuwa chanzo cha ajali hiyo ni wakati basi la abiria lililokuwa likielekea mji mkuu wa Gulu lilipogonga lori lililokuwa limeengeshwa barabarani huku likipakiwa mizigo. Watu mbalibali sasa wanasema kuwa uzembe wa madereva ndio sababu ya ongezeko hili la ajali - hasa wale wa magari ya abiria wanaotaka kufanya safari nyingi wakati huu ambapo watu wengi wanasafiri kutoka au kuelekea vijijjini:

Takwimu za polisi zinaonesha kuwa kati ya ajali 206 zilizotokea katika kipindi cha hadi mwishoni wa mwaka, watu walipoteza maisha yao katika ajali 47 zilizosababishwa na makosa ya madereva na pia watu wanaotembea kwa miguu kutozingatia usalama wao.

Hata hivyo, kuna baadhi ya raia wanaoelezea kuwa vitendo vya ulaji rushwa miongoni mwa polisi wa usalama barabarani navyo vinachangia kwa ajali hizo. Magari ya abiria yana ratiba za safari ambazo waendeshaji wengi hawazizingatii alimuradi watawapa polisi kitu kidogo.

Aidha, katika kipindi cha likizo ya Krisimasi, inadaiwa kuwa kuna watu wanaojinunulia magari kama njia ya kuonesha mafanikio yao mwaka huo bila kuwa na uzoefu.