1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yajivunia ongezeko la ndovu

26 Agosti 2015

Uhifadhi wa tembo Nchini Uganda umeleta tabasamu nyusoni mwa wapenzi wa wamyamapori. Utafiti unaonyesha kuwa tembo hao ni zaidi ya 5000 huku mataifa mengi barani Afrika yakisalimu amri kwa wawindaji haramu.

https://p.dw.com/p/1GLZc
Afrikanischer Elefant lange Stoßzähne Kenia Afrika
Picha: picture alliance/dpa/S. Meyers

Ni nembo ya ufahari wa Afrika....lakini sasa imegeuka kuwa ishara ya uhalifu na ulafi miongoni mwa wanadamu. Kila baada ya saa moja tembo watatu wanauliwa na wawindaji haramu.

Huku tembo wakiendelea kuangamia kupitia mtutu wa bunduki, Uganda inamuagiwa sifa kutokana na ufanisi wake wa kuwahifadhi. Taifa hilo linajivunia ongezeko la asilimia 600 ya wanyama hao miongo michache iliyopita.

"Inaonyesha kuwa panapokuwa na usimamizi mzuri wa sheria na msaada wa kiufundi, inawezekana kuzuwia kupungua kwa wanyama tunakoshuhudia katika baadhi ya meneo mengine. Bado kuna sehemu chache ambako idadi ya tembo inaongezeka," amesema Simon Hedges kutoka shirika la kuhifadhi wanyama pori.

Utafiti waonyesha

Kwa mujibu wa utafiti uliyofadhiliwa na mwanzilishi mwenza wa Shirika la Microsoft Pul Allen, Uganda imepiga hatua kubwa kuwahifadhi tembo.Kufikia sasa wanyama hao ni zaidi ya 5000 idadi ni ya juu ikilinganisha na tembo 700 miaka ya thamanini.

"Pongezi ziwaende maafisa wa misitu wa Halmashauri ya kulinda wanyama pori kwa kutekeleza wajibu wao bila uwogo. Kazi wanayoifanya bilashaka ni hatari, " anasema Michael Keigwin afisa wa shirika la kuhifadhi wanyama pori la Uganda.

Kenia Elefanten
Picha: picture-alliance/Woodfall/Photoshot/M. Hill

Mafanikio ya Uganda ni kinyume kabisaa na kushindwa vibya kwaTanzania ambako idadi ya tembo imepungua kwa asilimia sitini miaka mitano iliyopita. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika lisilo la kiserekali la Uingereza linalosimamia mazingira, Magenge haramu ya Wachina yanashirikiana na maafisa mafisadi nchini Tanzania kusafirisha viwango vikubwa vya pembe za ndovu.

"Miaka ishirini iliyopita ni bandari chache tu zilitumiwa kuendesha biashara haramu ya uwindaji wanyama pori. Lakini sasa ni maelfu. Mahitaji kutoka China yamechangia ongezeko la uwindaji haramu unaofanywa kwa ustadi, hivyo basi tunahitaji kubadili mbinu ya kukabiliana nao," Michael Keigwin anasema

Mambo yamebadilika

Historia ya Uganda kuhusu uhifadhi wa wanyama pori imekuwa ya kupigiwa mfano kutoka miaka ya 1960,ambapo wanyama wakubwa kama tembo na viboko walikuwa wengi kuliko ilivyokua katika mataifa mengine Afrika. Lakini mambo yalibadilika wakati wa utawala wa kiimla wa Idi Amin na kuzorota hata zaidi vikosi vya Tanzania vilipomg'oa mamlakani.

Hata hivyo msururu wa mikakati iliyowekwa miongo miwili iliyopita imeweza kunusuru kuangamia kwa tembo Nchini humo. Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori ya Uganda imefanyiwa mageuzi ili kupambana na wawindaji haramu ipasavyo.Ni mazingira hayo tulivu ndiyo yamechangia tembo kutoka mbuga ya kitaifa ya Virunga Nchini Congo kuvuka na kuingia Uganda.

"Bilashaka kuna tembo wanaohama kutoka katika mbuga virunga lakini karibu pande tatu zinaonyesha wazi kwamba ongezeko hili halitokani tu na uhamiaji huo. Tunaangazia ongezeko halisi," Simon Hedges.

Bunge la Uganda linajadili mswada ambao ukiidhinishwa kuwa sheria itatoa adhabu kali kwa wale watakaopatikana wakifanya biashara ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori.

Ni matumaini ya wengi kuwa Taifa hilo la afrika mashariki litaendela kuwa kielelezo chema na makao salam kwa tembo hawa.

Muandishi: Ambia Hirsi

Mhariri:Iddi Ssessanga